Home » » PILAU LA UBINGWA LANUKIA MSIMBAZI…SIMBA SC YAIPIGA 3-0 NDANDA NA KUREJEA KILELENI LIGI KUU

PILAU LA UBINGWA LANUKIA MSIMBAZI…SIMBA SC YAIPIGA 3-0 NDANDA NA KUREJEA KILELENI LIGI KUU


Mshambuliaji wa Simba SC, Ibrahim Hajib (kushoto) akimfunga tela beki wa Ndanda FC, Paul Ngalema katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Simba ilishinda 3-0
Beki wa Ndanda, Aziz Sibo akimzuia kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto jana Uwanja wa Taifa
Kiungo wa Simba, Jonas Mkude (kulia) akimiliki mpira mbele ya beki wa Ndanda, Aziz Sibo
Mshambuliaji wa Simba, Danny Lyanga akipasua katikati ya wachezaji wa Ndanda
Mshambuliaji wa Simba, Mussa Mgosi kulia akipambana na beki wa Ndanda jana Uwanja wa Taifa
Kiungo wa Simba, Awadh Juma akimlamba chenga beki wa Ndanda jana Uwanja wa Taifa


KAMA ilivyotarajiwa, Simba SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 3-0 jioni ya leo dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shukrani kwao, wafungaji wa mabao hayo, kiungo Mwinyi Kazimoto Mwitula kipindi cha kwanza na mshambuliaji Mganda, Hamisi Friday Kiiza mawili kipindi cha pili.
Simba SC sasa inafikisha pointi 51 baada ya kucheza mechi 22 na kuwashushia nafasi ya pili, mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 50 za mechi 21.
Simba walipata bao lao la kwanza dakika ya 35, baada ya Kazimoto kutuliza vizuri krosi ya Ibrahim Hajib iliyowapita kipa wa Ndanda, Jeremiah Kisubi na mabeki wake na kufumua shuti la kiufundi la juu lililotinga nyavuni.
Hamisi Kiiza akishangilia na wachezaji wenzake leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kufunga mabao yaliyoirejesha juu Simba

Mshambuliaji wa Uganda, Kiiza akaipatia Simba bao la pili dakika ya 57 kwa kichwa akimalizia kona ya Hajib, hilo likiwa bao lake la 17 msimu huu katika Ligi Kuu na kumfikia mshambuliaji wa Yanga, Mrundi Amissi Joselyn Tambwe aliyekuwa anaongoza.
Kiiza akafunga bao lake la 18 msimu huu wa Ligi Kuu dakika ya 73 na kumpiku Tambwe, akimalizia pasi ya mshambuliaji Danny Lyanga aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Jeremiah Kisubi kufuatia shuti kali la mpira wa dhabu la kiungo Mzimbabwe, Justive Majabvi.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Mbeya City
Imeifunga 2-0 Stand United Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, mabao ya Raphael Daudi na Haruna Shamte. 
Kikosi cha Simba kilikuwa; Vicent Angban, Hassan Kessy, Novaty Lufunga, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto/Mwinyi Kazimoto dk75, Jonas Mkude, Hamisi Kiiza, Ibrahim Hajib/Daniel Lyanga dk69 na Said Ndemla/Awadh Juma dk54. 
Ndanda FC: Jeremia Kisubi, Aziz Sibo, Paul Ngalema, Salvatory Ntebe, Hemed Khoja, William Elias, Omega Seme/Bryson Raphael dk46, Omar Mponda/Salum Mineli dk62, Atupele Green na Kiggi Makassy/Ahmed Msumi dk77.
Toa maoni yako kwa habari hii kwa kuweka email yako hapa,na endelea kutufatilia zaidi Ukurasa wa habari

0 comments:

 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger