Home » » USAJILI; SIMBA YAWEWESEKA KWA MESSI

USAJILI; SIMBA YAWEWESEKA KWA MESSI

          
                 



Akizungumza kwenye makao makuu ya klabu hiyo, Msimbazi jijini Dar es Salaam, ofisa habari wa Simba, Haji Manara alisema klabu yao imeamua kumwaga mboga baada ya kuona inafanyiwa hujuma.


Dar es Salaam. Kimya kingi kina mshindo! Ndicho unachoweza kusema baada ya uongozi wa Simba kuibuka na kueleza kuwa utaishtaki Azam FC kutokana na kumshawishi kwa lengo la kumsajili Ramadhani Singano ‘Messi’ pamoja na kuponda usajili uliofanywa na wapinzani wao kwa Malimi Busungu.

Akizungumza kwenye makao makuu ya klabu hiyo, Msimbazi jijini Dar es Salaam, ofisa habari wa Simba, Haji Manara alisema klabu yao imeamua kumwaga mboga baada ya kuona inafanyiwa hujuma.

“Sisi Simba, sasa imetosha, kama watu wanaamua kumwaga ugali, sisi tunamwaga mboga, hatutaki kuyumbishwa,” alisema Manara kwa jazba huku akieleza kuwa muda wa kuyumbishwa kwa klabu yao umepita.

Hivi karibuni, Messi alihusishwa na kufanya mazungumzo ya kujiunga na Azam.

Kuhusu hilo, Manara alisema wanatafuta ushahidi ili kuishtaki klabu pinzani ambayo ilifanya mazungumzo na mchezaji huyo.

“Tumesikia kuna klabu imefanya mazungumzo na mchezaji wetu, Messi ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja, kama inamtaka ije tuipe dau letu, lakini si kuitana kinyemela.

Akijibu shutuma hizo, Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba alikanusha madai ya kufanya mazungumzo na Messi na kueleza kuwa haina mpango wa kumsajili nyota huyo wa Simba.

Sababu za kumkosa Busungu

Simba katika mchakato wa kupata saini ya mshambuliaji Malimi Busungu wa Mgambo JKT aliyejiunga na Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita na kumkosa.

Hata hivyo, Manara alibainisha kuwa ilimwacha nyota huyo ambaye alitaka fedha ambazo haziendani na thamani ya kiwango chake uwanjani.

“Tulimwambia ukweli Busungu kuwa kama ana nia ya kucheza Simba, dau letu ni Sh5 milioni, yeye akahitaji Sh40 milioni, fedha ambazo tulimwambia hatuwezi kumpa kwani hajafikia kiwango hicho,” alisema Manara.

Naye mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Simba, Zacharia Hanspoppe aliwaponda Yanga kiaina baada ya kudai kuwa wao hawataki kusajili wachezaji wanaovuma, bali wanasajili kwa kuangalia mahitaji ya timu.

Alisema anajua kuwa wengi wanataka kuona Simba ikisajili wachezaji wenye majina makubwa na wanaovuma hivi sasa, lakini wao hawaangalii hilo, wanachoangalia ni ubora wa mchezaji na mahitaji ya kikosi chao kwanza.
“Sisi wala hatutaki kushindana na mtu katika kusajili, eti huyu kasajili huyu na sisi tusajili yule, hilo kwetu halipo, tunachofanya ni kusajili kulingana na timu inahitaji nini kwa wakati huo,” alisema Hanspoppe.
“Timu yetu bado ni nzuri, inakosa mambo madogo madogo, hivyo tunachofanya ni kukiongezea nguvu katika nafasi ambazo tumeona zimepwaya na wala hatutaki kusajili mchezaji kwa sababu jina lake linavuma, tunasajili mchezaji tunayemhitaji na siyo anayevuma,” alisema Hanspoppe.
Rage ahusishwa sakata la Messi
Klabu ya Simba imekuwa katika marumbano na mshambuliaji wake, Ramadhan Singano ‘Messi’ ambaye anadai kughushiwa kwa mkataba wake. “Mkataba wa Messi tumeurithi kwa uongozi uliopita (mwenyekiti alikuwa Ismail Aden Rage) na walimsajili kwa mkataba wa miaka mitatu, leo hii anadai alisaini miaka miwili. “Dole gumba na saini ni ya Messi na tulipomuuliza alisema alisainishwa na Mzee Kinesi (Joseph Itang’are), niweke wazi kuwa Simba haijawahi na haiwezi kughushi mikataba ya mchezaji yeyote,” alisema.
Alisema klabu hiyo imeunda kamati maalumu kuchunguza jambo hilo na itachukua hatua stahiki baada ya uchunguzi wao kukamilika.
Yamtupia virago Amri Kiemba
Akizungumzia usajili wa mchezaji Amri Kiemba ambaye Azam aliyokuwa akiichezea kwa mkopo imeeleza dhamira ya kumrudisha ilikomtoa (Simba), Manara alisema klabu hiyo haina mpango na mchezaji huyo.
“Hatuna mpango wa kumrudisha Kiemba, hatuna nafasi hiyo,” alisema Manara ambaye hakuwa tayari kuweka wazi kama mkataba wa mchezaji huyo na klabu hiyo umemalizika au la.
Madeni yanayoikabili klabu
“Nakiri ni kweli tunadaiwa, lakini hakuna taasisi duniani ambayo haidaiwi, hata Marekani, nchi tajiri inadaiwa, sembuse Simba, tunajipanga ili kulipa madeni hayo,” alisema Manara.
Alikiri kuwa klabu yao inadaiwa na baadhi ya wachezaji wake iliyovunja nao mikataba, Amissi Tambwe na Donald Mosoti.

Ujio wa kocha mpya na usajili
Akizungumzia kazi ya usajili na kocha mpya, Manara alisema, kocha mpya atatangazwa ndani ya siku nne kuanzia jana baada ya uongozi kukamilisha mchujo wa makocha walioomba kuinoa timu hiyo.
“Usajili tunaendelea vizuri, na kweli nilikwenda kwenye mashindano ya Cosafa (Afrika Kusini) ili kuangalia wachezaji, mchakato utakapokamilika kila kitu kitawekwa wazi, tutasajili kutokana na mahitaji yetu msimu ujao na upungufu tuliokuwa nao msimu uliopita ,” alisema.
Toa maoni yako kwa habari hii kwa kuweka email yako hapa,na endelea kutufatilia zaidi Ukurasa wa habari

0 comments:

 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger