Home » » MAWAZIRI ZANZIBAR WASUSIA BAJETI

MAWAZIRI ZANZIBAR WASUSIA BAJETI

 
Zanzibar. Mawaziri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na Wawakilishi kutoka CUF jana walitoka kwenye kikao cha bajeti cha Baraza la Wawakilishi, wakipinga urasimu katika utoaji vitambulisho vya ukazi wa Zanzibar na uandikishaji wapigakura.
Muda mfupi baada ya tukio hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilitoa taarifa yake ikisema kitendo cha mawaziri wa CUF kutoka kwenye kikao cha bajeti ni kuvunja katiba, kwa kuwa wameshindwa kuheshimu kiapo cha utii katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Mawaziri hao walitoka nje ya kikao hicho muda mfupi baada ya Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Juma Duni Haji kusimama na kutoa malalamiko ya kutoridhishwa na utendaji wa SUK katika kusajili na kutoa vitambulisho hivyo vinavyotumika katika kuandikisha wananchi kwenye Daftari la Wapigakura.
Wakati wawakilishi hao wanaondoka ndani ya ukumbi, wenzao wa CCM walikuwa wakipiga makofi huku wakiimba “CCM, CCM, CCM”, na baadaye baraza kuendelea na muswada wa kupitisha mapato na matumizi ya bajeti ya mwaka 2015/2016.
Mawaziri waliohudhuria mkutano huo ni Abubakar Khamis Bakar ambaye ni Waziri wa Sheria na Katiba, Fatma Abdulhabib (Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais), Abdilahi Jihadi Hassan (Mifugo na Uvuvi) na Haji Mwadini Makame (Ardhi, Makazi, Maji na Nishati).
“Tumeamua kutoka ndani baada ya kuona wenzetu tuliowaamini, wametubadilikia. Hawana nia njema ya kuendesha serikali ya pamoja,” alisema makamu mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji alipoongea na waandishi baada ya kutoka kwenye ukumbi huo.
“Wameanzisha Serikali ndani ya Serikali na sasa wanawanyima haki wananchi kinyume na katiba.”
Duni alisema kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakizungushwa kusajiliwa na kupewa vitambulisho vya ukazi, hali inayowaweka katika hatari ya kupoteza haki zao za kijamii, ikiwa ni pamoja na fursa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, alisema uamuzi wao haujavunja katiba ya Zanzibar na kwa hiyo wataendelea na shughuli za Serikali kama kawaida.
Alidai kuwa kazi ya uandikishaji wapigakura kwenye Wilaya ya Magharibi, Unguja imetawaliwa na vitisho na kwamba watu wasiojulikana wamekuwa wakionekana wakiwa na silaha za moto na kujifunika vitambaa usoni mithili ya maninja na wengine kuvaa vinyago.
“Katika maisha yangu sijawahi kuona askari anayekwenda kulinda akificha uso na huu ni mkasa mpya duniani. Huwezi kumlinda raia kwa silaha za moto wakati yeye hana chochote zaidi ya mikono yake,” alisema Duni.
Naibu katibu mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema kuna vijana wamekwama kuandikishwa na kuitaka Serikali kuondoa urasimu katika upatikanaji wa vitambulisho vya ukazi.Alisema amechunguza na kubaini kuwa kuna vijana walio na umri chini ya miaka 18 ambao wanaandikishwa kwenye kambi tatu za jeshi ambazo hakuzitaja na baadaye kupewa vitambulisho ili waandikishwe katika Daftari la Wapigakura.
Taarifa ya SMZ
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud inasema hatua ya mawaziri kutoka ndani ya chombo hicho inakwenda kinyume na kiapo cha kulinda na kutetea Katiba ya Zanzibar na kimeitia doa SUK.
Alisema haikuwa muafaka kususia kupitisha Bajeti Kuu ya serikali wakati walishiriki katika kupanga na kuitayarisha kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri na kitendo hicho ni kwenda kinyume katika uwajibikaji wa pamoja. “Lengo lao kubwa ni bajeti ishindwe kupita ili serikali ishindwe kutoa huduma kwa wananchi. Bahati nzuri bajeti imepita lakini sisi kama viongozi tusichanganye siasa na utekelezaji wa shughuli za serikali tutairudisha nyuma Zanzibar na kuwaingiza wananchi katika matatizo,” alisema.
Alisema uandikishaji wapigakura na usajili wa vitambulisho vya Mzanzibari hufanyika kwa kuzingatia sheria na katiba kama kuna kasoro walitakiwa kuziwasilisha katika mamlaka zinazohusika.
Alisema malalamiko yanayotolewa hayana msingi wala nguvu ya hoja kwa sababu Tume ya Uchaguzi (ZEC)inaongozwa na makamishina kutoka vyama vya siasa, ambavyo ni pamoja na CCM na CUF na hakuna malalamiko yaliyowahi kutolewa.
Waliosalia wawananga
Akichangia hoja ya bajeti, waziri wa zamani na mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma aliiomba Serikali iongeze muda wa siku tano apate nafasi ya kuwasilisha hoja binafsi ili wananchi waulizwe kama bado wanataka kuendelea na SUK au warudi kwenye mfumo wa zamani.
Alisema kitendo kilichofanywa na mawaziri kususia shughuli za Serikali ndani ya Baraza ni uvunjaji wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo waliapa kuilinda na kuitetea wakiwa viongozi wakuu wa Serikali.
Alisema kwamba kwa kuwa wao ni mawaziri na wamegoma kufanya kazi, wanapaswa kukabidhi magari ya Serikali na kumtaka Rais wa Zanzibar kutumia mamlaka aliyopewa kikatiba kuchukulia hatua suala hilo.
“Hata kama rais atawaacha, katiba tayari imewafukuza na sasa wanapaswa waache magari ya Serikali na wakafanye kazi nyingine Mtendeni. Haiwezekani wanakula sambusa, keki Ikulu baadaye wanapinga kazi za serikali kinyume na viapo vyao,” alisema Hamza huku akishangiliwa na wajumbe waliosalia.
Alisema lengo la kuundwa SUK ilikuwa ni kujenga umoja, kuondoa chuki na ndio maana Rais aliyepita, Amani Abeid Karume aliipigania SUK kama njia ya kurejesha amani na utulivu kwa wananchi wa Zanzibar.“Wenzetu wameamua kuanzisha vurugu lazima tukae upya tuangalie kama kuna sababu ya kuendelea na mfumo wa serikali ya pamoja. Yanayotokea sasa ni kinyume na malengo ya kuletwa kwa mfumo wa serikali ya pamoja,” alisema.
Wajumbe wengine waliochangia ni Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Amali, Ali Juma Shamhuna aliyesema mawaziri hao walisusia kikao bila ya kuwa na hoja ya msingi.
“Mheshimiwa Spika, wenzetu waliahidi kuondoa matatizo mbalimbali kwa bajeti zao za mwaka huu, ikiwamo suala la ukosefu wa taa kwenye Uwanja wa Ndege wa Pemba, leo wanasusia kupitisha bajeti kuu, wanataka maendeleo au hawataki?” alihoji.
Taarifa ya CUF
Baadaye CUF ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikiilaumu ZEC kwa kuendelea kuandikisha watu kwenye Daftari la Wapigakura licha ya kuwapo kasoro nyingi.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alieleza katika taarifa hiyo kuwa uandikishaji umekumbwa na vurugu zilizotokana na kutumika kwa vyombo vya dola vinavyolazimisha watu wasio na sifa kuandikishwa.
Alisema: “CUF inaeleza kwamba vitambulisho 109 vilikataliwa kutambuliwa na mashine za BVR, lakini masheha na vikosi vya Serikali walilazimisha watu kuandikishwa.
“Tume ya Uchaguzi ilikataa kutoa idadi ya askari waliohamia kutoka maeneo mengine, huku watu wakipigwa na kukamatwa, wakiwamo waliokwenda katika vituo vya polisi kuwawekea dhamana wenzao waliokamatwa,” inasema taarifa hiyo.CHANZO:MWANANCHI
Toa maoni yako kwa habari hii kwa kuweka email yako hapa,na endelea kutufatilia zaidi Ukurasa wa habari

0 comments:

 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger