MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi
(CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, leo amechukua fomu na kutangaza nia ya
kugombea urais kupitia chama hicho huku akiahidi kuunda serikali ya
umoja wa kitaifa kukabiliana na ufisadi.
Mbali na kuunda serikali ya umoja wa
kitaifa, amesema ataweka lengo binafsi la kuongoza nchi kwa haki ili
aweze kuwa rais wa kwanza wa Tanzania kushinda tuzo ya uongozi uliotukuka na wenye mafanikio kwa marais wa Afrika, ‘Tuzo ya Mo Ibrahim’.
Hii inatajwa kuwa tuzo kubwa zaidi
duniani kwani mshindi hupatiwa fedha ikilinganishwa na tuzo nyingine
duniani. Tuzo hii ilianzishwa mwaka 2007.
Prof. Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti mweza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) amekabidhiwa fomu hiyo na Mohamed Mkandu, Katibu wa CUF wilaya ya Kinondoni, baada ya kulipia gharama ya Sh. 500, 000.
Prof. Lipumba ametangaza nia ya kuutaka
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mbele ya Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambaye pia ni Katibu Mkuu
wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, viongozi wa chama na maelfu ya
wananchama wa chama hicho.
Tofauti na ilivyotarajiwa ukumbi huo
ulifurika wafuasi wa chama hicho hali iliyopelekea wengine kubaki nje ya
ukumbi wakisubiri angalau kumuona kiongozi wao.
Lipumba amesema “nimechukua fomu kupitia
chama changu kama ambavyo utaratibu unataka. Kisha kama UKAWA wataniona
nafaa watanipendekeza kugombea urais.”
Amesema iwapo UKAWA itampitisha kuwania
urais, serikali watakayoiunda itahakikisha maoni ya wananchi,
yaliyonyofolewa na Bunge Maalum la Katiba lililoongozwa na CCM
yanarejeshwa hasa katika vipengele vya mfumo wa muungano, uadilifu na
uwajibikaji.
“Tatizo la ufisadi linachangiwa na
viongozi kupewa zawadi. Rasimu ya wananchi ikiweka kifungu kinachowataka
viongozi kutoa taarifa na kuzikabidhi zawadi hizo serikalini, lakini
mafisadi wamekiondoa kifungu hichi.
Aidha, amesema Bunge hilo liliondoa
kipengele cha viongozi watanzania kutoruhusiwa kuwa na akaunti za benki
nje ya nchi ili kuepuka uibaji wa fedha zinazofichwa nje ya nchi. Hali
ambayo inachochea vitendo vya kifisadi kuendelea kushamili.
Amesema tatizo ni matumizi mabaya ya
fedha za umma na ufisadi uliokithiri. Katika ripoti Ripoti ya Mdhibiti
na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow
ameonesha makosa ya jinai ya kughushi nyaraka na kukwepa kodi.
“Makosa yapo wazi, lakini mpaka hivi sasa
waliohusika hawajafikishwa mahakamani. Na wengine waliochota fedha hizo
wanazitumia kutafuta wadhamini ili wagombee urais kwa tiketi ya CCM,”
amefafanua Prof. Lipumba.
“Kama nitapewa ridhaa na Ukawa, sina
mswalia Mtume na mafisadi. Nitahakikisha uwazi, uwajibikaji na uadilifu
ziwe ni tunu za taifa,” ameeleza Prof. Lipumba.
Ameeleza pia atahakikisha matatizo ya
ukosefu wa lishe kwa watoto yanakoma ikiwa ni sehemu ya kujenga taifa
imara, kuhakikisha haki ya uzazi salama, ujenzi wa miundombinu,
uwezeshwaji wa watoto wa kike ikiwemo kukomesha mimba za utotoni,
kumaliza magojwa ya malaria na kifua kikuu na kuanzisha hifadhi ya
wazee.
“Katika kila watoto 100 watoto 42 wana
udumavu unaosababishwa na kutopata lishe bora. Ukimnyima mama na mtoto
lishe bora nikuwanyima maendeleo.
“Lazima akina mama wapate fursa ya
kujifungua salama. Tutahakikisha tunawapa fursa watoto wa kike ili
kujiendeleza kielimu,” ameeleza Prof. Lipumba.
Prof. Lipumba amesema, “Hivi sasa tayari
kuna matatizo ya panya road ni kwa sababu ya kukosa ajira na kukosa
matumaini . Ni lazima tujenge mazingira ya kuwapatia watanzania ajira za
kutosha.”
Aidha, Hamad amesema Tanzania ipo tayari
kwa mageuzi, watanzania wamechoka na ukandamizaji. Na ili kuyapata
mabadiliko hayo ni lazima wafanye maamuzi kwa kutumiaUKAWA.
Akitaja sifa za Rais, Hamad amesema,
“hatakiwi kuwa mbinafsi, ayaweke matatizo ya wananchi rohoni na moyoni,
mwenye upeo mkubwa wa kuona mambo, kujenga uchumi imara na madhubuti,
mwenye mawazo mapya, ahakikishe rasilimali zote zinawanufaisha
watanzania wote.”
Prof. Lipumba
aliyewahi kuwa mshauri wa masuala ya uchumi wa Rais wa awamu ya pili,
Ali Hassan Mwinyi alizaliwa 6 June 1952, Ilolangulu, Tabora. Ni
Mwanasiasa na Mchumi wa kimataifa. Ameoa mke mmoja. Mwaka 1959 – 1966
Alisoma elimu ya msingi.
Mwaka 1967 – 1970 alisoma Shule ya
Sekondari ya wavulana ya Tabora na kuhitimu elimu ya kidato cha sita
mwaka 1972 katika Shule ya Sekondari ya Pugu ambapo mwaka 1973 alijiunga
na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisomea uchumi ngazi ya
Shahada.
Mwaka 1978 alitunukiwa shahada ya pili ya
uchumi baada ya masomo ya uchumi chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwaka
1978 alijiunga Chuo Kikuu cha Marekani cha Stanford ambapo alisoma
uchumi na kutunukiwa PHD.
0 comments:
Post a Comment