Mwenyekiti wa MOAT Reginald Mengi
Ukweli ni kuwa kila binadamu ana haki ya kupata maendeleo anayoyahitaji, ili kukuza na kustawisha utu wake.
Uhuru wa habari ni kati ya haki muhimu za binadamu ambazo zinatambuliwa na dunia nzima kikatiba. Watu wa habari tunaamini kwamba ‘hakuna maendeleo bila habari.’
Ukweli ni kuwa kila binadamu ana haki ya kupata maendeleo anayoyahitaji, ili kukuza na kustawisha utu wake.
Mungu alimuumba mwanadamu kwa uhuru na matakwa yake, hivyo Mungu anamshirikisha mwanadamu uhuru huo ili amtambue, amtumikie, amsifu na kumwabudu.
Kwa hivyo, kukosekana au kuminywa kwa uhuru wowote ule, uwe wa kisiasa, wa uchumi wa kuabudu (dini), kifkra, kiutamaduni na hasa uhuru wa habari, ni kuwafanya watu kuwa wendawazimu.
Kama kuna kitu mwanadamu yeyote anakipigania kwa akili zote na nguvu zote, basi ni uhuru ambao ni haki ya msingi ya kila mwanadamu.
Katiba Inayopendekezwa inasema: “ Kila mtu ana haki na uhuru wa kutafuta, kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa sahihi.
Ibara hiyo inaendelea kusema kwamba kila mtu ana uhuru wa kuanzisha vyombo vya habari na njia nyingine za upashanaji habari.
Miswada ya habari
Wakati ibara hiyo imewekwa vizuri katika katiba hiyo, miswada miwili inayokaribia kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete inabomoa uhalisia huu.
Muswada umetengeneza mazingira magumu ya upatikanaji wa habari pamoja na usambazaji wake.
Mimi kama mwanahabari, najiuliza hivi Serikali yetu ina malengo gani na tasnia ya habari? Je, ina lengo la kuboresha au kukandamiza uhuru wa habari hasa kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu?
Nikiwa nchini Ghana, niliwahi kusoma habari za malalamiko mengi kuhusiana na miswada hii miwili ya habari.
Muswada mmoja unahusu upatikanaji wa habari na wa pili unahusu
usimamizi wa vyombo vya habari. Ni kweli uhuru bila mipaka pia ni
uwendawazimu.
Viongozi wa dini
Gazeti moja la kila siku lilieleza habari za
viongozi wa dini hususani maaskofu wa Kanisa Katoliki na Baraza la
Waislamu waliokutana, ili kujadili kadhia hiyo inayohusu uhuru wa habari
nchini katika dunia hii ya ukuaji wa tasnia ya habari.
Kabla ya viongozi hawa wa dini kukutana na
kujadiliana kero hii, tayari wabunge hasa wale wa upinzani walishatoa
kauli zao za kutokubaliana na sheria hizo ambazo zinalenga kukandamiza
uhuru wa habari nchini, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi
Mkuu Oktoba 2015.
Viongozi hao wanatamka wazi kwamba iwapo miswada hiyo itaisainiwa na Rais, nchi hii itageuka ya kidikteta kama enzi za mkoloni.
Kwa kawaida, ukiona viongozi wa dini ambao ni
wasomi, wenye busara na wanaoongozwa na uchaMungu wanakutana kujadili
masuala ya jamii, ujue kwamba jambo hilo Serikali imepoteza mwelekeo.
Kwa mfano, viongozi wa dini walionya mapema juu ya
upungufu katika mchakato wa katiba mpya, lakini Serikali ikapuuzia; na
leo matokeo yake kura ya maoni imesitishwa.
Gharama zilizotumika katika mchakato huo ni kubwa kupindukia. Wahenga wanasema: ‘asiyesikia la mkuu huvunjika guu.’
Wadau wengine wa habari wameshatoa maoni yao na
kuitaka Serikali kurekebisha upungufu uliomo katika miswada hii ya
habari, lakini hata hivyo Serikali inaonekana kushikilia msimamo wake.
Wamiliki wa vyombo vya habari nchini chini ya
uenyekiti wa Reginad Mengi nao wametoa maoni yao na hofu yao juu, lakini
je, Serikali itasikiliza vilio vya wadau hao?
Baadhi ya sheria zilizomo katika miswada hiyo hakika ni kinyume kabisa cha ukuzaji wa uhuru wa habari.
Kwa mfano, kuwadai waandishi wa habari kuwa na
digrii ya kwanza kama kigezo cha kuwa mwandishi wa habari, ni
kuikandamiza habari.
Je, ni kwa nini digrii ianze na waandishi na si wabunge,
mawaziri au madiwani? Wakati Serikali ikiweka masharti magumu kwa
waandishi wa habari, inasemekena sifa ya mtu kugombea ubunge ni kujua
kusoma na kuandika.
Kibaya zaidi sheria hizi kwa nini zilingoja hadi
kipindi hiki cha mwisho cha uongozi wa awamu ya nne tena kipindi cha
kuelekea uchaguzi mkuu? Je, wananchi wapate picha gani kuhusu sheria
kandamizi kama hizi?
Tafsiri ya wananchi wengi ni kwamba Serikali
imeshikwa pabaya katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, ndiyo kwa maana inakuja
na sheria kandamizi kwa uhuru wa habari ili kuwanyima wananchi habari
sahihi kuhusiana na uchaguzi huo.
Je, huku ndiyo kukua kwa demokrasia na utawala bora nchini Tanzania, kama tunavyojigamba katika medani za kisiasa?
Kwa upande mwingine, kama yalivyo masuala mengine
ambayo yameleta migogoro katika jamii, hili nalo limeongeza mgogoro
mwingine kwa serikali pamoja na wadau wa habari, wanahabari na pia
viongozi wa dini.
Hivi nikisema miswada hii ni kitanzi kingine cha
serikali ya CCM nitakuwa nimekosea? Je, viongozi wa dini wakiingilia
kati watakuwa wameiingilia Serikali katika utendaji wake?
Viongozi wa dini wanashuhudia kwamba pole pole
uhuru wa habari unapotea katika jamii yetu kwa masilahi binafsi ya
wanasiasa wachache. Madhehebu ya dini yanamiliki pia vyombo vya habari,
navyo vikubali kukandamizwa? Namuomba Rais Kikwete kutafakari kwa kina
madhara ya kusaini miswada hii. Akumbuke kuwa hata chama chake hakiwezi
kupona sheria hii ikipita.
Chanzo;MWANANCHI
Chanzo;MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment