Home » » MAKALA;CCM HAIWEZI KUTEUA MGOMBEA URAIS MUADILIFU

MAKALA;CCM HAIWEZI KUTEUA MGOMBEA URAIS MUADILIFU

 
> Wanachama na Washabiki wa chama cha Mapinduzi wakiwa katika moja ya shughuli za chama hicho.Makada wengi wa chama hicho wamejiatokeza  kutangaza nia ya kugombea urais.Picha na Maktaba. 
Na Profesa Ibrahim Lipumba


Wamesafirisha wapambe nchi nzima. Bila haya wanawaeleza wananchi kuwa waliohudhuria mkutano huo wamejilipia wenyewe gharama za safari.


Wagombea urais kupitia CCM wanachukua fomu za chama hicho. Baadhi yao wamefanya kufuru za matumizi ya mbwembwe za kutangaza nia ya kugombea urais.

Wamesafirisha wapambe nchi nzima. Bila haya wanawaeleza wananchi kuwa waliohudhuria mkutano huo wamejilipia wenyewe gharama za safari.

Televisheni na redio zimerusha matukio haya moja kwa moja kwa gharama kubwa. Baadhi ya wagombea hawana fedha na hawakuweza kufanya mbwembwe nyingi. Wanaopigiwa chapuo la kupata uteuzi wa CCM ni wale wenye fedha nyingi. Ufisadi umekuwa mfumo wa CCM. Asiyekuwa na fedha hawezi kushinda uteuzi.

Ufisadi wa CCM ulidhihirika katika mchakato wa kujadili Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

Katiba Inayopendekezwa imeondoa mambo muhimu yaliyokuwemo ndani ya rasimu ambayo ni matokeo ya maoni ya wananchi. Moyo wa Rasimu ya Katiba ya wananchi ni mfumo wa Muungano wa shirikisho la serikali tatu. Rasimu ya Katiba ilitenganisha utekelezaji na usimamizi wa mambo ya Muungano na mambo ya Tanganyika.

Tume ya Jaji Warioba ilipendekeza mfumo wa shirikisho ili kuondoa kero za Muungano na kuondoa “utata wa aina na muundo wa Muungano ambao umesababisha kuvunjwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Serikali zote mbili mara kadhaa.”

Tume imeeleza historia ya utata wa mfumo wa Muungano tangu mwaka 1984 palipotokea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa’ na kusababisha aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, kujiuzulu.

Rasimu ya Katiba ilikusudia kuondoa dhana ya Tanganyika kuvaa koti la Muungano kwa kutenganisha mambo ya Muungano na mambo ya Tanganyika.

Kwa mfano, Serikali ya Muungano imechanganya ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika wizara moja. Jeshi la Kujenga Taifa si jambo la Muungano. Zanzibar wana Jeshi la Kujenga Uchumi. Kabla ya kuteuliwa kuwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Wananchi, Jenerali Davis Mwamunyange alikuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa. Lakini haiwezekani Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi la Zanzibar akawa CDF.

Mafisadi hawapendi kutenganisha mambo ya Tanganyika na mambo ya Muungano, kwa sababu yanaondoa fursa ya Rais wa Muungano na wapambe wake kuifisidi nchi.

Tunu muhimu za kuzingatia katika kuongoza na kusimamia mambo ya nchi na umma ni pamoja na uwazi, uwajibikaji na uadilifu. Kuhakikisha kuwa Bunge linaisimamia na kuiwajibisha serikali Rasimu ya Katiba ilipendekeza wabunge wasiwe mawaziri. Wabunge wasiionee haya Serikali kwa sababu miongoni mwao ni mawaziri. Rais siyo sehemu ya pili ya Bunge. Jambo hili limewekwa kapuni katika Katiba Inayopendekezwa. Mamlaka ya Rais kuweza kuiendesha nchi kidikteta yamebakia ndani ya Katiba Inayopendekezwa. Misingi ya uadilifu wa viongozi uliowekwa katika sura ya tano ya Rasimu ya Katiba imeondolewa. Ibara ya 15 (1) ya Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba inaeleza:

“Kiongozi wa umma wakati anapotekeleza shughuli za kiserikali, akipewa zawadi, zawadi hiyo itakuwa ni mali ya Jamhuri ya Muungano na ataiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara au kiongozi wa taasisi ya Serikali inayohusika, akiainisha: (a) aina ya zawadi; (b) thamani ya zawadi; (c) sababu ya kupewa zawadi; na (d) mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo. (2) Neno ‘zawadi’ kama lilivyotumika katika ibara hii linajumuisha kitu chochote chenye thamani atakachopewa kiongozi wa umma katika utekelezaji wa shughuli za umma. (3) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.” Katiba Inayopendekezwa imekiondoa kifungu hiki.
Kifungu hiki kiliondolewa maksudi ili kulinda maslahi ya mafisadi. Wakati Bunge Maalum linajadili Rasimu ya Katiba, baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu walipokea zawadi za fedha zilizochotwa kutoka akaunti maalum u ya Tegeta. Hawakuzitolea taarifa wala kulipa kodi.
Tanzania haitakuwa ya kwanza kuweka kifungu kama hiki katika katiba. Katiba ya Nigeria Ibara ya 6 (3) iunaeleza “Zawadi yoyote itakayotolewa kwa mtumishi wa umma akiwa katika shughuli au sherehe ya kiserikali itachukuliwa kuwa zawadi iliyotolewa kwa taasisi ambayo mtumishi wa umma husika anaiwakilisha.”
Ibara ya 16 ya Rasimu ya Katiba ya jaji Warioba inaeleza “Kiongozi wa umma - (a) hatafungua au kumiliki akaunti ya benki nje ya Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu; na (b) hataomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma.” Kifungu hiki pia kimeondolewa.
Sababu ya mapendekezo ya ibara hii ni kuzuwia viongozi na watumishi waandamizi wa umma kufungua akaunti nje ya nchi na hasa katika mfumo wa benki za maficho zilizopo katika nchi za Uswisi, kisiwa cha Jersey na Isle of Man.
Hali hii inaashiria kuwa viongozi au watumishi hao waandamizi wamejipatia fedha hizo kwa njia zisizo halali na pia husababisha kudhoofika kwa vyombo vya fedha nchini.
Itakumbukwa katika uchunguzi wa kashfa ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE, gazeti la kila siku la Uingereza ‘The Guardian’, lilieleza kuwa makachero wa taasisi inayoshughulikia ufisadi mkubwa ya Uingereza (United Kingdom Serious Fraud Office) yaligundua kuwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, alikuwa na akaunti yenye zaidi ya dola milioni moja katika kisiwa cha Jersey Uingereza.
Waandishi wa habari walipomuuliza suala hili aliieleza kuwa hivyo “vijisenti” vina maelezo yake. Taarifa hii ilithibitisha wazi kuwa kuna mtandao katika maafisa wa juu wa serikali ambao wana fedha nyingi kwenye akaunti nje ya nchi ambazo zimepatikana kwa njia zisizoeleweka.
Karibu wagombea wote wa CCM walikuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Hamna hata mmoja aliyepinga vifungu vya Rasimu ya Katiba vinavyoimarisha uwazi uwajibikaji na uadilifu visiondolewe.
Kati ya wagombea hawa, yeyote akiwa Rais ataendeleza ufisadi. Kuin’goa CCM ni jambo la lazima ili tupambane na ufisadi.
CHANZO;MWANANCHI
Toa maoni yako kwa habari hii kwa kuweka email yako hapa,na endelea kutufatilia zaidi Ukurasa wa habari

0 comments:

 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger