Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru
Mwanasiasa
mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru (Pichani) amesema
anahisi kuna mchezo mchafu unapangwa kwenye mchakato wa kupata mgombea
wa urais wa chama hicho tawala, akitaja idadi kubwa ya waliojitokeza
kuwa ni ishara mbaya.
Mwanasiasa
huyo mkongwe aliyefanya kazi na marais wa awamu zote nne, pia, bila
kumtaja jina, alitumia muda mwingi kwenye hotuba yake kujibu kauli ya
makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula aliyekaririwa akisema kuwa
mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi.
Kingunge,
ambaye amejitokeza hadharani kumpigia debe Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa alionyesha hofu hiyo jana wakati mbunge huyo wa Monduli
alipokuwa akihitimisha kazi ya kusaka wadhamini mkoani Dar es Salaam
kwenye ofisi za CCM Mkwajuni wilayani Kinondoni.(P.T)
Hadi
sasa, makada waliochukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya CCM ni 41
baada ya mwanachama mmoja kuchukua fomu jana akisema atamudu kupata
wadhamini kwa njia ya mtandao katika siku tano zilizosalia. Akizungumza
katika mkutano wa kusaka wadhamini ulioandaliwa kwa ajili ya Lowassa
wilayani Kinondoni jana, Kingunge alipingana na kauli ya Mangula kuwa
mgombea wa CCM atanadiwa na chama, si kujinadi mwenyewe akisema chama
hicho kinataka mgombea anayekubalika ndani na nje.
Siku tatu
zilizopita, Mangula alihojiwa na kituo cha televisheni cha Shirika la
Utangazaji Tanzania(TBC) na kusema mgombea wa chama hicho hatakiwi
kujinadi mwenyewe, kusisitiza kuwa anatakiwa kunadiwa na chama.
Lakini
Kingunge aliikosoa kauli hiyo jana akisema chama hicho kimeweka
utaratibu na hakuna sababu ya kuuacha na kuanza kuwahukumu wagombea
kabla ya vikao na kusisitiza kuwa CCM haikuwahi kuwahukumu wagombea
kabla katika chaguzi zilizopita.
“Mchakato
ufuate taratibu zilizowekwa,” alisema Kingunge ambaye aliibuka
Kinondoni ambako Lowassa alimalizia shughuli zake jijini Dar es Salaam.
“Nimemsikia
kiongozi wetu mmoja tena juzi juzi hapa, nikamuona kwenye televisheni
anasema mtu hawezi kwenda kujinadi yeye binafsi, ananadiwa na chama.
“Nikasema
eh! hilo hilo. Lakini nataka nimweleze yeye na wenye fikra kama hizo
kuwa kuna ngazi mbili katika utaratibu wetu; kwanza, mwanachama
anayetaka kuwania ubunge, udiwani, urais lazima ajinadi ndani ya chama,
ndivyo tulivyofanya miaka yote kwa mujibu wa katiba na taratibu zetu.
Ndivyo wanavyofanya sasa wakina Lowassa.”
Alisema pili, wagombea wakishajinadi chama kitamteua mmoja ambaye kitamnadi na yeye ataendelea kujinadi.
“Si
vizuri watu ambao tumewapa vyeo katika chama wakaanza ama wakaendelea
kukitumia chama chetu kwa mambo yao binafsi. Kama wana mashaka tupo
tunaojua mambo ya chama,” alisema Kingunge huku akishangiliwa na mamia
ya watu.
Kingunge
alisema mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa Dodoma alisema
chama kinatafuta mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama hicho ili
kuweza kushindana na vyama vingine.
“CCM
inamtafuta mtu ambaye anakubalika ndani na nje ya chama. Wale wanaofanya
jitihada za kuunda mazingira ya kukitafutia chama kushindwa, wanataka
historia iliyotukuka ya CCM iishe katika awamu ya nne,” alisema.
”Tunapozungumzia
suala la urais kwa sababu linahusu watu, tusianze kukaa kwenye
mizengwe. Kwanza tuwaulize watu wanamtaka nani atayeweza kuwatatulia
matatizo yao.”
Kingunge
alisema idadi ya wagombea nafasi ya urais waliojitokeza kwa tiketi ya
CCM ni wengi na kwamba idadi hiyo ambayo alisema haijapata kutokea
katika historia ya chama, inaashiria kuwa kuna jambo linataka kufanyika.
“Nasema
hao wagombea wapo wengi, sasa wenye macho wanaona watu wanasema nini.
Matumaini yangu ni kwamba watu watatuliza vichwa kukubali ukweli na
kuachia utaratibu wetu uendelee unavyotakiwa,” alisema.
Aliwataka
viongozi ndani ya CCM kutokiuka taratibu za chama hicho za kumteua
mgombea, kuwataka kutumia utaratibu uliozoeleka na ambao ulitumiwa
katika chaguzi zilizopita.
Alisema
Watanzania wana changamoto nyingi na kwamba tangu mwanzo chama hicho
kimekuwa kikilia na umasikini unaolikabili taifa, huku akisisitiza kuwa
mwarobaini wa kuondoa hali hiyo ni Lowassa.
Kingunge alisema licha ya marais wa awamu zote kufanya mambo mengi, nchi kwa sasa inahitaji kiongozi atakaye ondoa umaskini.
“Na
linawezekana hilo, nasema tunapozungumzia suala zima la urais
tunazungumzia hatma ya Watanzania. Tusifanye mchezo nalo, hatuwezi kukaa
tukasema yeyote tu anaweza. Hiyo sio lugha ya watu makini. Kauli hiyo
itasemwa na walionacho, lakini wasionacho hawawezi kusema hivyo,”
alisema Kingunge.
Kauli ya Lowassa
Akizungumza
kwa nyakati tofauti akiwa wilayani Ilala, Temeke na Kinondoni jijini
Dar es Salaam, Lowassa alirejea kauli iliyotolewa na Mwalimu Julius
Nyerere ya mwaka 1995, kwamba watu wanataka mabadiliko na wakiyakosa
ndani ya CCM, watayatafuta nje ya chama hicho.
“Mimi
nitayaleta haya mabadiliko nikiwa ndani ya CCM. Nagombea urais kwa
sababu nauchukia umasikini na nitaunda serikali ya kusaidia wanyonge,
kuwafukuza machinga, mamantilie na waendesha bodaboda ni upuuzi. Watu
wanatafuta riziki tunawafukuza inatakiwa tuwawekee mazingira mazuri,”
alisema na kushangiliwa kwa nguvu.
Alisema
anauchukia msongamano wa magari jijini Dar es Salaam na iwapo atakuwa
Rais atalimaliza tatizo la foleni katika jijini Dar es Salaam kwa miezi
sita.
“Kutakuwa
na waziri anayeshughulika na jiji la Dar es Salaam tu kama ilivyo kwa
nchi jirani ya Kenya. Yeye akiamka tu akili yake yote ni kushughulikia
changamoto za jiji hili,” alisema Lowassa ambaye mara kwa mara alikuwa
akiwaimbisha wananchi wimbo wa ‘mchakamchaka’, huku akisisitiza kuwa
ataiongoza serikali yake kwa mtindo wa mchakamchaka akisema ambaye
hataweza atakaa pembeni.
Aliwataka
wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la
Wapigakura ili wapate fursa ya kumchagua iwapo atapitishwa na chama
hicho kugombea urais, huku akiwataka wamuombee kwa maelezo kuwa Mungu
ndiye anayepanga kila kitu.
“Mrema
(Augustine) alikuwa maarufu sana mwaka 1995 mpaka gari lake likawa
linasukumwa na wananchi, lakini katika kura za urais hakushinda.
Jiandikisheni ili tufanikishe safari ya matumaini,” alisema.
Lowassa
alisema kutokana na idadi kubwa ya wananchi wanaomuunga mkono anaona
kama tayari ameshashinda huku akisisitiza kuwa ameshawafunga goli
wagombea wenzake kama anavyofanya mchezaji wa timu ya soka ya Real
Madrid, Cristiano Ronaldo.
“Kati ya wagombea wote hakuna mwenye uzoefu ndani ya CCM kama mimi. Kumbukeni rais ndiye mwenyekiti wa CCM,” alisema.
Aiteka Dar
Lowassa aliwasili katika uwanja wa ndege wa zamani (Terminal 1), saa 2:00 asubuhi akitokea mkoani Arusha.
Mwenyekiti
wa CCM wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida alisema wanachama wa mkoa
huo waliojitokeza kumdhamini ni 212,150, kati yao kutoka Kinondoni ni
95,251, Temeke (72,100) na Ilala (44,799).
Afananishwa na mtume, Yesu
Akimkaribisha
Lowassa Dar es Salaam, Madabida alimfananisha waziri mkuu huyo wa
zamani na Mtume Muhammad ambaye alikuwa akitangaza dini lakini alikuwa
akipingwa na watu wake wa karibu na kufafanua kuwa kutokana na hali hiyo
Mungu alimueleza kuwa hatamuacha na atakuwa pamoja naye.
0 comments:
Post a Comment