Home » » JE WAJUA? KILA MTANZANIA ANADAIWA LAKI 8

JE WAJUA? KILA MTANZANIA ANADAIWA LAKI 8

 
Kambi rasmi ya upinzani bungeni imesema Serikali inatakiwa kukusanya Sh19.6 trilioni kwa mwaka tofauti na malengo iliyojiwekea ya Sh13.4 trilioni, huku ikihoji sababu za miradi ya maendeleo kutegemea mikopo ambayo alisema imeongeza ukubwa wa deni kwa wananchi.
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti Mbadala jana, Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia alisema lengo hilo linaweza kufikiwa endepo Serikali itaweka mazingira mazuri na rafiki kwa mlipakodi.
Mbatia, aliyeingia kwa staili ya aina yake akionyesha mkoba uliobeba bajeti, alisindikizwa na Mchungaji Peter Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, Moses Machali (Kigoma Kasulu), Salum Barwani (Lindi Mjini) na Mustapha Akonay (Mbulu).
Mbatia alitaja njia nyingine za kuongeza mapato kuwa ni kupunguza misamaha ya kodi isiyokuwa na tija hadi kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa, kuongeza ufanisi Bandari ya Dar es Salaam na kuweka mazingira mazuri na endelevu katika sekta ya utalii.
Mbatia alirejea wito wa kila mwaka wa wapinzani wa kutaka juhudi zaidi kuwekwa katika kupanua wigo wa vyanzo vya mapato katika sekta kama uvuvi, maliasili, nyumba na ardhi.
Alisema Serikali ipanue wigo wa kodi, kuweka sera na viwango vya kodi vinavyotabirika na endelevu, kuongeza ufanisi wa TRA kwa asilimia 50 na kudhibiti ukwepaji wa kodi.
“Tutaweza kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi hadi kufikia asilimia 20 mpaka 25. Washindani wetu wakubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki wanakusanya mapato kwa asilimia 22 ya Pato la Taifa, na hawana mazingira mazuri ya uwekezaji na rasilimali nyingi kama Tanzania,” Mbatia.
Mbatia aliendelea kubainisha sura ya bajeti mbadala kuwa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yatakuwa ni Sh18 trilioni na mapato ya halmashauri kuwa Sh848.1 bilioni.
Alisema mikopo na misaada ya kibajeti ni Sh660 bilioni huku mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo ikiwa ni Sh1.6 trilioni.
Msemaji huyo wa Kambi ya Upinzani alilinganisha bajeti ya Serikali na bajeti mbadala na kusema bajeti mbadala haina mikopo ya kibiashara, hivyo inalenga kulipunguzia taifa mzigo wa madeni.
“Bajeti ya Serikali ina mikopo ya kibiashara ya asilimia 10, bajeti hii inawaongezea wananchi mzigo wa madeni,” alisema Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Alisema hivi sasa kila Mtanzania anadaiwa Sh873,904.56 kutokana na deni la Taifa kuzidi kukua.
Toa maoni yako kwa habari hii kwa kuweka email yako hapa,na endelea kutufatilia zaidi Ukurasa wa habari

0 comments:

 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger