Mvutano mkali ulioibuka jana katika kikao cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, umesababisha kushindwa kumtaja mgombea wake wa urais.
Kutokana na mvutano huo, viongozi wa vyama hivyo
waliahirisha kikao hicho na kuitisha mkutano na waandishi wa habari na
kueleza kuwa watamtangaza mgombea huyo Jumanne ijayo.
Kikao hicho kilichowahusisha wabunge wote na
viongozi wakuu wa vyama vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi
vinavyounda Ukawa, kilifanyika jana katika ukumbi wa Millenium, Dar es
Salaam.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alishindwa kuwaeleza wanahabari kilichowakwamisha kumtangaza mgombea,
huku akisisitiza kuwa wanataka kuweka mambo sawa.
“Hatuwezi kuwaangusha Watanzania na kipindi hiki
ndiyo chetu kwani tunaingia katika uongozi wa Serikali ili kulikomboa
taifa,” alisema: “Kuna mambo ya kukubaliana na kuweka sawa, tutamtaja
mgombea wetu Julai 14 (keshokutwa). Naomba niwaeleze Watanzania kuwa
Ukawa haiwezi kuvunjika tunachokifanya ni kuwa makini katika maamuzi
yetu.”
Alisema kikao cha Kamati ya Ukawa kilifikia
muafaka na jana kuwasilisha mrejesho kwa wabunge ndipo ulipofikiwa
muafaka wa kusubiri hadi keshokutwa, huku akisisitiza kuwa katika
kugawana majimbo wamekubaliana kwa asilimia zaidi ya 90.
Alipobanwa aleleze ni mambo gani yaliyokwamisha
kufikiwa kwa muafaka alisema: “Kuna mambo ya kujadiliana baina ya vyama
vyetu ila hayawezi kuleta matatizo, tupo pamoja na tutatoa jibu la
pamoja.”
Alisema Ukawa imetokana na maoni ya wananchi
kuhusu Katiba Mpya, hivyo kiongozi atakayepitishwa na chama hicho lazima
awe, mwadilifu, muwazi na mwajibikaji.
“Lazima tuwe na mgombea atakayesimamia mambo ya
wananchi waliyotaka yawemo katika Katiba, mambo hayo ni yale yaliyowekwa
katika rasimu ya Katiba ya Jaji (Joseph) Warioba,” alisema Profesa
Lipumba.
Alisema kama katiba ya nchi ingekuwa na kifungu
kinachoruhusu vyama kuungana, vyama vinavyounda Ukawa vingeungana lakini
kutokana na sintofahamu hiyo katika Katiba, wanalazimika kutatua
changamoto hiyo kwa umakini mkubwa.
Kuhusu majimbo alisema; “ni kama tumeshagawana
yote isipokuwa ambayo yana wagombea wawili wawili, yaani kutoka vyama
zaidi ya viwili. Tumekubaliana majimbo zaidi ya 170 mpaka sasa.”
0 comments:
Post a Comment