MAAZIMIO YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA CHAMA KATIKA
KIKAO CHAKE CHA TAREHE 2 – 3 APRILI, 2016 KILICHOFANYIKA MAZSONS HOTEL,
MJINI ZANZIBAR
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama Cha Wananchi) limefanya kikao chake cha kawaida kwa siku
mbili, tarehe 2 hadi 3 Aprili, 2016 mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi ya Chama, Mheshimiwa Twaha Taslima.
Ajenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni Hali ya Kisiasa
Zanzibar na mwelekeo wa CUF baada ya kufanyika kile kilichoitwa uchaguzi
wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016.
Baada ya kupokea na kujadili kwa kina ajenda hiyo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:
1. Linawapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa
ujasiri, uzalendo na ari kubwa walioionesha kwa kuitikia kwa kiasi
kikubwa wito wa chama chao cha CUF wa kuwataka wasishiriki katika uhuni
na ubakaji wa demokrasia uliopewa jina la uchaguzi wa marudio wa tarehe
20 Machi, 2016.
Baraza Kuu la Uongozi limefurahishwa kuona zaidi ya
asilimia 80 ya wapiga kura wa Zanzibar hawakujitokeza kushiriki katika
uchaguzi huo haramu na batili, na hivyo kuudhihirishia ulimwengu kwamba
Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina ridhaa ya wapiga kura hao.
2. Linawapongeza waliokuwa wagombea wa CUF kwa
nafasi zote za Urais, Uwakilishi na Udiwani kwa kuheshimu maamuzi ya
Chama na kutoshiriki uchaguzi haramu na batili wa marudio licha ya njama
nyingi zilizokuwa zikifanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar chini ya
Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, za kulazimisha ushiriki wao. Msimamo
wa wagombea hao umewadhihirishia na kuwathibitishia CCM kwamba tofauti
na wao, viongozi wa CUF hawajali nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka
ni kuleta mabadiliko ya kweli kwa maslahi ya watu wote wa Zanzibar.
3. Linawapongeza kwa namna ya pekee wagombea Urais,
Uwakilishi na Udiwani wa vyama vyengine vya upinzani ambavyo ni UMD,
JAHAZI ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP, na ACT-WAZALENDO, na vile
vinavyoshirikiana kupitia UKAWA ambavyo ni CHADEMA, NCCR na NLD
vilivyoungana na wananchi wa Zanzibar kususia uchaguzi haramu na batili
wa marudio na kusimamia maamuzi halali ya wapiga kura waliyoyafanya
kupitia uchaguzi mkuu halali wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
4. Linazishukuru na kuzipongeza jumuiya na taasisi
zote za kitaifa na kimataifa pamoja na nchi rafiki za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambazo zilikataa kuleta waangalizi wa uchaguzi
katika uchaguzi huo haramu na batili na hivyo kuungana na Wazanzibari
katika kutetea maamuzi yao halali waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu
halali uliokuwa huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
5. Linavishukuru na kuvipongeza vyombo vya habari
vya ndani na nje ya nchi pamoja na waandishi wa habari na wapiga picha
kwa jinsi vilivyosaidia kuonesha ulimwengu uchaguzi mkuu uliokuwa
halali, huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia kwa jinsi
vilivyoanika uchafuzi wa tarehe 20 Machi, 2016 hasa kule kuonesha vituo
vya kupigia kura vikiwa havina watu na hivyo kuwasaidia Watanzania na
ulimwengu kuujua ukweli ambao CCM na Tume yao ya Uchaguzi walikuwa
wakijaribu kuuficha.
6. Linalaani tabia na mwenendo wa uongo, uzushi, na
uvunjwaji wa Katiba, Sheria na Maadili wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, dhidi ya matakwa na maamuzi halali ya
Wazanzibari waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu huru na wa haki wa tarehe
25 Oktoba, 2015 na kitendo chake cha kuiingiza Zanzibar katika dimbwi
la chuki, uhasama, uvunjifu wa haki za binadamu na udhalilishaji wa raia
kwa sababu tu ya kukiridhisha chama chake cha CCM ambacho kimekataliwa
na Wazanzibari.
Vitendo vya Jecha Salim Jecha vimeishushia hadhi Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar na kuichafulia jina Zanzibar na Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania mbele ya jumuiya ya kimataifa na kuonekana haiko tofauti na
nchi nyengine za Afrika zisizoheshimu matakwa na maamuzi ya wananchi
katika uchaguzi.
7. Linalaani hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli kuleta nguvu kubwa ya vikosi vya
ulinzi na usalama kuja kubaka demokrasia Zanzibar.
Baraza Kuu linalaani vikali nguvu kubwa iliyotumiwa na
vyombo vya dola dhidi ya raia wasio na hatia kwa lengo na madhumuni ya
kuwatisha na kuwazuia wasitumie haki zao za msingi kama ibada kwa
kuwalazimisha kutotoka nje ya nyumba zao kuanzia saa 2 usiku wakati muda
huo ni muda wa ibada ya sala kwa Waislamu ambao ni asilimia 99 ya
wananchi wote wa Zanzibar.
Baraza Kuu pia linalaani mwenendo wa viongozi wa juu wa
vyombo vya ulinzi na usalama wa kutumika waziwazi kisiasa kwa kuegemea
upande wa CCM na kuwakandimiza viongozi na wanachama wa CUF kinyume na
maadili ya kazi zao.
8. Linalaani vitendo vya Serikali kuunda makundi ya
kiharamia ambayo yamekuwa yakiwahujumu raia wasio na hatia yakitumia
silaha za moto na silaha za kienyeji huku yakitumia gari za Idara Maalum
za SMZ.
Baraza Kuu linalaani Jeshi la Polisi ambalo limekuwa
likiyalinda makundi haya na kutochukua hatua zozote dhidi yao licha ya
wananchi wanaohujumiwa kutoa taarifa kwa jeshi hilo.
Badala yake, katika matukio mengi Polisi imewageuzia kibao wananchi waliohujumiwa kwa kuwakamata na kuwaweka ndani.
Baraza Kuu linawataka Wakuu wa Jeshi la Polisi kujirudi,
kutekeleza majukumu yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao na na
kufuata maadili yao na kuwacha kujifanya ni Idara ya Polisi ya CCM.
9. Haliyatambui matokeo ya uchaguzi huo haramu na
batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa
Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa Wawakilishi na wala
haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani.
Baraza Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa
kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na
Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa na watu hao.
CUF haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni
kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na
haikutokana na ridhaa ya watu.
Kwa vyovyote vile, Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa
ya Katiba ya Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa
Katiba ambayo inaeleza kwa uwazi kabisa namna ya kuundwa kwa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
10. Linawataka wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za
amani, za kikatiba na kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi
nyingine duniani kuwakataa watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu
waliojiweka madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa
kutoipa ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.
11. Linaendelea kuutambua uchaguzi mkuu uliokuwa halali,
huru, wa haki na uliofanyika katika hali ya amani na utulivu wa tarehe
25 Oktoba, 2015 na pia linayatambua matokeo yake ambayo yalionesha wazi
kwamba chaguo la Wazanzibari ni CUF na Maalim Seif Sharif Hamad
kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Kitendo cha zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari kususia
uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016 kimezidi kuyapa nguvu
maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba, 2015 mbele ya macho ya Watanzania na
dunia.
12. Linaendelea kuwataka Wazanzibari kuwa watulivu na
kulinda amani iliyopo na linawahakikishia kwamba CUF inaendelea na
juhudi zake za kutafuta haki yao na kusimamia maamuzi yao waliyoyafanya
tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa njia za amani na za kidemokrasia. Njia hizo
za amani zimefanikiwa na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa ambayo
imeanza kuchukua hatua dhidi ya ubakwaji wa demokrasia uliofanyika.
13. Linazishukuru na kuzipongeza nchi washirika wa
maendeleo kwa kuchukua maamuzi ya kuzifutia misaada Serikali za
kidikteta za CCM ambazo zimebaka demokrasia na kukanyaga haki za
wananchi wa Zanzibar.
Baraza Kuu linatoa wito kwa nchi hizo washirika wa
maendeleo na jumuiya za kimataifa kuchukua hatua zaidi dhidi ya Serikali
za CCM na madikteta wake walioshiriki katika ubakaji wa demokrasia
Zanzibar zikiwemo hatua makhsusi dhidi ya watu makhsusi waliohusika na
ubakaji huo wa demokrasia na uvunjaji wa haki za binadamu katika kipindi
hiki.
MWISHO, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
linawahakikishia wanachama wake wote na Watanzania kwa ujumla kwamba
chama chao kiko imara na hakitoyumba wala kuyumbishwa katika kutetea na
kupigania haki zao hadi tutakapofanikisha ujenzi wa taifa imara
linalosimamia na kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu,
demokrasia na utu wa watu wote.
0 comments:
Post a Comment