James Mbatia.
Wakati
kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikianza kupitia ripoti ya
IPTL kuhusu uchunguzi wa ufisadi katika Akaunti ya Tegeta Escrow,
wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umedai kwamba kuna
mikakati imeandaliwa kuzima ripoti hiyo kusomwa na kujadiliwa bungeni.
Mwenyekiti
mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema jana kwamba moja ya mikakati hiyo
ni madai ya kuwapo barua ya Mahakama kuzuia mjadala huo akisema mkakati
huo unatokana na ukubwa wa kashfa na jinsi inavyowahusisha viongozi
waandamizi serikalini.
Mbatia
aliyeambatana na kundi kubwa la wabunge kutoka Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi, alisema: "Iko mikakati na mbinu za kila aina kulihujumu
Bunge lisisimamie fedha za walipakodi, ndiyo maana kuna danadana na tuna
taarifa za kuwapo barua kutoka mahakamani kuzuia jambo hilo
lisijadiliwe bungeni kwa madai eti kuna kesi.
"Mahakama
haiwezi kuingilia shughuli za Bunge, inatia wasiwasi kwa kuwa Ofisi ya
Bunge nayo imekuwa na danadana kila siku kwa kubadilisha badilisha
ratiba wakati sisi tunataka hawa waliohusika kwenye kashfa hii
wachukuliwe hatua."
Pia, alisema kuna taarifa kwamba Serikali inadai haina fedha, ikitaka kufupisha Bunge na suala hilo lisijadiliwe sasa hivi.
Mbunge wa
Mkanyageni (CUF), Mohammed Mnyaa alisema: "Serikali inategesha tegesha
tu mambo bungeni na ndiyo maana leo (jana) wameahirisha Bunge hadi kesho
(leo) bila sababu za msingi, wanafinya muda wa sisi kujadili sakata
hili," alisema Mnyaa.
Mnadhimu
Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alisema escrow ni kama ilivyokuwa
kashfa ya Richmond ambayo iliwang'oa wahusika wakuu bungeni, hivyo
haiwezekani isijadiliwe bungeni kwa madai kwamba Mahakama imezuia...
"Hakuna utaratibu kama huo wa Mahakama kuelekeza Bunge kitu gani kifanyike na gani kisifanyike pia hata Katiba hairuhusu hilo."
Lissu
alishangazwa na Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha Bunge jana hadi leo
kwa madai kuwa yeye (Lissu) alikuwa hajakamilisha taarifa ya upinzani
kwenye muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka
2014 akidai kuwa huo ni upotezaji wa muda.
"Nilimwomba
Naibu Spika kuwa aahirishe muswada huo hadi kesho kwa kuwa ulikuwa
umepangwa tarehe 25 lakini ghafla ukabadilishwa na mimi sikuwapo kwa
muda wote huo. Sikuomba aahirishe Bunge nilimwomba aahirishe muswada
tu," alisema Lissu.
Mwenyekiti
wa PAC, Zitto Kabwe alisema naye amesikia kuwapo barua ya Mahakama
kuzuia mjadala huo na kusema kama ni kweli, halitakuwa sahihi.
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara katika Operesheni Delete CCM mjini Dodoma
jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema si Waziri Mkuu
wala Jaji Mkuu anayeweza kuuzima mjadala wa escrow bungeni.
Alisema
kashfa hiyo ambayo chama chake kina nyaraka zake na ripoti za uchunguzi
wa escrow na Takukuru, lilianzia bungeni na lazima lijadiliwe na
kumalizikia bungeni.
Ndugai ajibu hoja
Akizungumzia
madai hayo, Ndugai alisema hajui kama kuna barua kutoka mahakamani
kuzuia mjadala wa escrow bungeni na suala hilo litawasilishwa na PAC
bungeni Novemba 27 kama ilivyopangwa.
"Waiamini
kamati, kwanza hawa wa upinzani ni yao (kamati) haiongozwi na CCM, mimi
naamini kamati itafanya kazi nzuri. Sidhani kama kanuni zinaruhusu
kugawa ripoti hiyo kwa kuwa ni siri, kanuni hairuhusu."
Rejea
Ripoti ya
Tegeta Escrow inatokana na uchunguzi maalumu wa Sh306 milioni
zilizochotwa katika akaunti ya escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
Fedha
hizo zilitokana na gharama za uwekezaji zilizokuwa zinalipwa na Kampuni
ya Kufua Umeme ya IPTL baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina ya
wabia hao.
Tanesco
ililalamika kuwa ilikuwa inailipa zaidi IPTL kinyume na gharama halisi
za uwekezaji, hivyo kuamuliwa na Mahakama kuwa fedha hizo ziwekwe katika
escrow hadi upatikane ufumbuzi wa mgogoro huo lakini zikachukuliwa
kabla kesi kuamuliwa.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment