LAZARO
Nyalandu-Waziri wa Maliasili na Utalii, ametamba kuwa Serikali
itapambana na ujangili hadi hapo majangili watakaposalimu amri.
Katika mwendelezo wa vita hiyo, Nyalandu ametangaza kukamatwa kwa silaha za kivita zikiwemo bunduki za AK 47 na SMG katika Pori la Akiba la Rungwa.
Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita,
majangili wamevamia kwa kasi na kuwaua wanyamapori wakiwemo tembo na
faru, hatua ambayo iliibua tishio la kutoweka kwa baadhi ya wanyamapori.
Silaha hizo zimekamatwa kutoka mikononi
mwa majangili, ambapo katika msako huo, majangili 10 yalikamatwa kabla
ya kukamilisha mipango ya kuua tembo ndani ya pori hilo.
Wakati alipoteuliwa kushika wadhifa huo,
Nyalandu alitangaza vita na mtandao wa ujangili akionya kuwa kamwe
hatarudi nyuma katika kulinda maliasili za taifa wakiwemo wanyamapori.
Akizungumza baada ya kukagua silaha zilizokamatwa, Nyalandu amesema serikali kamwe haitarudi nyuma hadi majangili wasalimu amri.
Alisema kukamatwa kwa shehena ya silaha
hizo nyingi zikiwa na kivita, ni salamu kwa majangili kuwa serikali iko
makini na inaendelea na mapambano.
Nyalandu amesema “silaha hizo zikiwemo SMG na AK47 zinatumika kwenye vita, lakini sasa majangili wanazitumia kuua tembo”.
Hata hivyo, amesema majangili hayo
yalidhibitiwa kabla ya kuua tembo na kwamba, watuhumiwa 10 walitiwa
mbaroni huku wananchi waishio jirani wakitoa ushirikiano mkubwa.
Amesema hakuna jangili nchini ambaye atakuwa salama iwapo hataweka silaha chini na kuwa, serikali ni lazima ishinde.
Amewaeleza askari na maofisa wa wizara
yake katika Pori la Rungwa kuwa, kukamatwa kwa silaha hizo ni ishara
kuwa ulinzi zaidi unapaswa kuimarishwa kwenye maeneo ya pembezoni.
Kwa mujibu wa Nyalandu, kwa sasa serikali itaelekeza nguvu zaidi katika mapori yalipo pembeni likiwemo la Rungwa.
Alisema kwa sasa askari wa wanyamapori
wanaendelea kupewa mafunzo maalumu ya kijeshi kwa lengo la kuwawezesha
kuwa na mbinu za kisasa zaidi za kupambana na majangili.
Alitangaza kuwa awamu ya pili ya mafunzo
hayo, askari wa wanyamapori watapatiwa mafunzo ya kikomandoo zaidi ili
kuwaongezea ukakamavu wa kupambana na majangili ambao wanaonekana
kutumia silaha kali zaidi.
Kaimu Meneja wa Pori la Rungwa, Kwaslema
Male, alimweleza Nyalandu kuwa silaha hizo zimekamatwa katika kipindi
cha kuanzia Januari 2012 hadi Aprili, mwaka huu, huku idadi kubwa zikiwa
zimekamatwa mwanzoni mwa mwaka huu.
Alizitaja silaha hizo kuwa ni AK 47 (2),
SMG (3), Bastola (38), gobore (263), risasi za AK 47 (28), risasi za SMG
(823) na misumeno ya kukatia miti kwa ajili ya mbao (197).
Male amesema “kwa sasa tumeimarisha doria
katika maeneo yote ya pori hilo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa
wananchi waishio jirani.
0 comments:
Post a Comment