Home »
» KINANA AKERWA NA UTITIRI WA KODI NCHINI
KINANA AKERWA NA UTITIRI WA KODI NCHINI
> Abdulrahaman Kinana
Moshi. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametaja utitiri wa kodi za Tanzania kama kikwazo cha wafanyabiashara kutofanikiwa.
Kinana alitoa kauli hiyo juzi kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Pasua mjini Moshi uliohudhuriwa na umati mkubwa wa watu.
Katibu huyo alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuwa na kodi nyingi ambazo hazina manufaa.
Alisema wafanyabiashara wanaumizwa zaidi na kodi hizo lakini hawana mtu wa kuwasemea zaidi ya kuendelea kunyonywa.
Hata hivyo, aliwatupia lawama wabunge wa CCM kuwa wingi wao bungeni hausaidii kitu kwa sababu wameshindwa kuondoa sheria zinazomkandamiza mwananchi.
“Kila kona ni kodi na kila kukicha ni kodi, Sumatra anadai kodi, Fire wanadai kodi, taasisi zingine zinadai kodi, yaani ni kero tupu,” alisema Kinana.
Katibu huyo alisema idara pekee inayotakiwa kudai kodi ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwani ndiyo waliobebeshwa dhamana ya kutafuta fedha.
Akizungumza na wafanyabiashara wakati wa chakula cha usiku, kiongozi huyo aliwataka kupaza sauti zao pale wanapohisi kuonewa.
Alitolea mfano wa Uganda kwamba wafanyabiashara waliigomea Mamlaka ya Mapato ya nchi hiyo hadi wakapelekana kwa Rais Yoweri Museveni.
“Sihamasishi wafanyabiashara mgome, lakini nasema hivi, hata Museveni aliwaambia URA kwamba ninaweza kubadiri idara za kodi lakini hawa wataendelea kulipa kodi, hivyo wafanyabiashara ni bora zaidi kuliko idara za kodi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kinana alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kulifungua soko la Kati ili wananchi waendelee na biashara zao.
Soko hilo lilifungwa tangu Machi, mwaka jana kwa madai ya kufanyiwa ukarabati mkubwa ingawa haujafanyika hadi sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alikubali kukutana na wafanyabiashara Aprili 9, mwaka huu, ili kupanga mkakati wa kuanza kufanyika kwa biashara sokoni hapo.
0 comments:
Post a Comment