Siku tano
baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa tamko la Jukwaa la Wakristo
(TCF) kuwataka waumini wao kupigia kura ya 'hapana' Katiba
Inayopendekezwa lilikuwa la hasira, viongozi hao wamejitokeza tena na
kusisitiza kwamba msimamo wao huo utabaki kama ulivyo.
Katika
tamko pamoja walilolitoa jana baada ya kukutana juzi mjini Dodoma,
viongozi hao wamemtahadharisha Rais Kikwete kuwa kuendelea kupigia debe
Katiba Inayopendekezwa na kuruhusu Mahakama ya Kadhi, kunaweza
kulitumbukiza Taifa katika machafuko na hali ikiwa hivyo Serikali ndiyo
itakayolaumiwa.
Tamko
hilo limesainiwa na viongozi walewale waliosaini lile la awali la Machi
12, mwaka huu ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa
Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa
Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.(P.T)
Tamko
hilo la maneno 921, limeendelea kuwataka waumini wao kujitokeza kwa
wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kuisoma
Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya
'hapana,' msimamo ambao tayari umeibua msuguano baina yao na Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo aliyesema viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuwaamulia waumini
wao aina ya kura wanayostahili kupiga.
Pia,
Jukwaa hilo limewataka viongozi wakuu wa Serikali –Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda na Rais Kikwete wasifurahi kwamba ujumbe wao umewafikia viongozi
wa dini waliozungumza nao hivi karibuni, kwa kuwa watu waliokutana nao
si wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa kutoa uamuzi au kukubaliana juu
ya jambo la kitaifa.
"Maaskofu
tuliokutana hapa (mjini Dodoma) hatuna hasira na wala hatuongozwi na
hasira wala mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya kama ambavyo
wengine wanavyotutafsiri, tunafikia maamuzi yetu baada ya maombi na sala
na tunasukumwa na upendo kwa wananchi ili kujenga Taifa lenye umoja,
amani, utulivu na maelewano," lilisema tamko hilo likihitimishwa kwa
maneno ya Biblia kutoka Mithali 29: 1, "Aonywaye mara nyingi akishupaza
shingo, atavunjika ghafla, wala hapati dawa."
Jumamosi
iliyopita, Rais Kikwete akifungua mkutano wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa
Dar es Salaam iliyoshirikisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali
ikijumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo, alisema msimamo wa
TCF kuhusu kuipigia kura ya 'hapana' Katiba Inayopendekezwa ni wa
hasira na usiokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa.
"Nimeyasoma
matamko hayo yote kwa umakini, imenishangaza, imenisikitisha na
kunihuzunisha. Siamini kwa nini wamefikia huko kwa kuunga au kutokuunga
mkono," alisema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete alisema: "Waacheni waumini waamue Katiba wanayoitaka wao... hayo
matamko niliyoyasoma yamejaa hasira kwa Serikali kupeleka bungeni
Muswada wa Mahakama ya Kadhi."
Maaskofu
hao walikuwa Dodoma kufuatilia kwa kina Muswada wa Marekebisho ya Sheria
mbalimbali ya mwaka 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine,
marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964
unaotambua Mahakama ya Kadhi.
"Muswada
huu unapendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi ambao utawasilishwa
bungeni leo kwa hati ya dharura na hivyo kuufanya umma wa Watanzania
kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo wakati bado hoja zetu za
msingi tulizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kwa
Waziri Mkuu hazijajibiwa," Ilieleza taarifa hiyo.
"Tunamtaka
Rais aagize muswada huu uondolewe bungeni na usijadiliwe tena kwa kuwa
utafiti wa Tume ya kurekebisha sheria ulishaonyesha madhara ya
uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi. Vinginevyo, kuendelea kujadiliwa kwa
muswada huu maana yake ni kwamba Serikali inajihusisha na itagharimia
mahakama hiyo."
0 comments:
Post a Comment