Ingawa aliingia madarakani kwa bashasha nyingi na
kauli mbiu zilizotia hamasa, lakini sasa anasema kazi ya urais ni ngumu
na anatamani amalize kipindi chake ili awe mtu huru.
Hotuba aliyotoa Rais Jakaya Kikwete, Oktoba 2014
alipokuwa Beijing, China ni kama alianza kuwaaga Watanzania akijiandaa
kustaafu urais.
Ingawa aliingia madarakani kwa bashasha nyingi na
kauli mbiu zilizotia hamasa, lakini sasa anasema kazi ya urais ni ngumu
na anatamani amalize kipindi chake ili awe mtu huru.
“Ni kweli naona kama muda hauendi kwa kasi ya
kutosha ili niweze kuwa raia wa kawaida na nipate muda wa kuchunga
ng’ombe na mbuzi wangu, nilime mananasi yangu kwa nafasi ya kutosha,”
alisema Rais Kikwete alipokuwa mkutanoni nchini China.
Kama ilivyo ada, kila anayemaliza ngwe yake huacha
kumbukumbu. Iwe mbaya au nzuri, swali ni je, yeye atakumbukwa kwa mambo
gani? Je, kuna watakaolia kwa furaha kuondoka kwake au watalia kwa
majonzi kwamba hawajui kesho yao?
Kikwete atakumbukwa kwa mambo makubwa na mazuri
aliyowafanyia Watanzania, lakini vile vile wapo watakaomkumbuka jinsi
alivyowaangusha kwa kutenda kinyume cha ahadi zake na kaulimbiu zake za
Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya au Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.
Watanzania wa kada mbalimbali wanazo sababu za
kumkumbuka Rais Kikwete atakapong’atuka madarakani. Hii itatokana na
jinsi walivyonufaika au kuumizwa kwa namna moja ama nyingine na utawala
wake.
Wanawake
Wanawake ni kati ya makundi katika jamii ambayo
kwa namna ya pekee watamkumbuka Rais Kikwete kwa jinsi alivyothamini
mchango wao na uwezo wao kiutendaji.
Ni katika awamu ya nne tangu ashike wadhifa huo,
alipoongeza kasi ya kuwaamini na akawateua kwa wingi baadhi yao kuingia
kwenye vyombo vya uamuzi kama uwaziri, ukuu wa mikoa na wilaya na nafasi
za uwakilishi kimataifa.
Katika kipindi chake, idadi ya majaji wanawake
iliongezeka, ikiwamo hata kufanikisha Anne Makinda kuwa mwanamke wa
kwanza kushika nafasi ya juu ya Spika wa Bunge. Je, atawaachia zawadi
wanawake kwa kupendekeza mmoja wao kuwa mgombea urais?
Vijana
Wazee
Wazanzibari
Wasomi
Wanachama wa CCM
Wakulima
Wananchi
Uchumi
Vyama vya upinzani:
Wanahabari
Vijana
Kundi hili nalo litakuwa na kila sababu ya kuhuzunika Kikwete
atakapoondoka madarakani. Hii ni kwa sababu kila alipofanya uteuzi,
hakuwaacha vijana.
Tangu alipojitosa katika kinyang’anyiro cha urais
kwa mara ya kwanza mwaka 1995, mkakati wake ulikuwa kuwapa vijana fursa
za uongozi na aliposhinda mwaka 2005 aliwateua bila hofu katika nyadhifa
mbalimbali.
Mifano ya vijana hawa ni kama January Makamba,
Lazaro Nyalandu, Mwigulu Nchemba (uwaziri); Lucy Mayenga, Halima
Dendegu, Wilmand Ndilu, Paul Makonda na wengineo (ukuu wa wilaya).
Wazee
Mbali na kuendelea kuamini busara za wazee, kila
alipotaka kutangaza jambo zito au kutoa hotuba ya mwisho wa mwezi
iliyotikisa nchi, alikutana na wazee ama Dar es Salaam au Dodoma, lakini
vile vile wazee wamo katika nafasi mbalimbali za uongozi; uwaziri, ukuu
wa wilaya na mikoa.
Wazanzibari
Rais Kikwete alijitahidi kadri ya uwezo wake kupatanisha wananchi wa Unguja na Pemba waliotofautiana kwa misingi ya siasa.
Chini ya ushawishi wake Wazanzibari walikubali
kuongoza nchi kwa ushirikiano; wakaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Uhasama uliondoka japokuwa kuna viashiria vya uhasama kurudi.
Wasomi
Hakuacha nyuma kundi la wasomi, kwani miongoni
mwao ndiyo wanaoongoza wizara nyeti na taasisi mbalimbali. Aliwateua
katika nafasi mbalimbali za uongozi japokuwa baadhi yao wamemwangusha.
Atakumbukwa alivyohamasisha ujenzi wa shule za
sekondari kukidhi ongezeko kubwa la wanaofaulu kutoka shule za msingi na
alivyojenga Chuo Kikuu cha Dodoma, upanuzi wa Chuo Kikuu Huria na vyuo
vya kati.
Wanachama wa CCM
Tofauti na vyama vingine vya siasa, CCM wanajivunia kumpata mtu
aliyekuwa kete ya ushindi kwa vipindi viwili mfululizo 2005—2010 na
2010—2015.
Watamkumbuka alivyowabeba, alivyofanyia
marekebisho katiba ya chama kuwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu kutoka
wilayani, alivyohuisha chama hadi kuwa na mvuto kuliko awali.
Hofu yao ni je, watampata mgombea ambaye atakuwa kete ya ushindi?
Wakulima
Kwa mara ya kwanza tangu Serikali ianze kuimba
wimbo wa kilimo ni uti wa mgongo, safari hii wakulima na wafugaji
walithaminiwa kiasi kwamba walipewa mbolea ya ruzuku, majosho na
alitatua migogoro ya ardhi na malisho japo kwa kasi ndogo.
Wananchi
Watamkumbuka alivyowapa vyandarua, alivyojenga
zahanati, vituo vya afya na alivyoongeza vifaa na majengo katika
hospitali kadhaa, hususan katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili;
vitengo vya upasuaji wa moyo na vinginevyo.
Kigoma watamfurahia alivyojenga daraja la Mto
Malagalasi pamoja na barabara ya kuunganisha na Mkoa wa Tabora; Kusini
watamkumbuka alivyokamilisha daraja la Umoja; alivyoongeza vivuko na
alivyofurukuta kukamilisha kipande cha kilomita 60 kutoka Ndundu hadi
Somanga katika barabara ya Dar es Salaam – Mtwara iliyoanza kujengwa
mwaka 1996.
Uchumi
Mabadiliko ya sheria ya uwekezaji angalau
yamewezesha nchi kuanza kunufaika na kodi ya uzalishaji, ingawa bado si
kwa kiasi kikubwa.
Ni katika utawala wa Rais Kikwete ambapo kumekuwa
na uboreshaji wa huduma za kibenki, mikopo ya saccos, uboreshaji wa njia
za uchukuzi kama barabara, vivuko, reli kwa kununua vichwa na mabehewa,
ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uwekezaji umeongezeka.
Vyama vya upinzani:
Miongoni mwa watakaolia kwa furaha ni wapinzani wakikumbuka
kiongozi huyo alivyoshindwa kujali haki za binadamu na ushahidi ni namna
Jeshi la Polisi lilivyotiririsha damu ya wapinzani wake kisiasa.
Mifano mingine ni alivyokimbilia kusuluhisha
mgogoro wa Kenya huku polisi wakilaza watu kwa risasi Mtwara kufuatia
mgogoro wa gesi; na Serikali yake ilivyoanzisha Operesheni Tokomeza
Ujangili iliyoishia kutiririsha damu ya watu wasio na hatia kama
wakulima, wafugaji na wawindaji lakini si majangili.
Wanahabari
Tasnia nzima ya habari kwa kiasi kikubwa,
itamkumbuka Rais Kikwete kwa jinsi Serikali yake ilivyonyonga uhuru wa
habari kwa kufungia magazeti kama Mwananchi, MwanaHalisi, Mtanzania,
Kulikoni na hivi karibuni The East African na zaidi askari polisi
walivyomuua mwanahabari Daudi Mwangosi chini ya utawala wake.
Kubwa zaidi kwa wanahabari ni kushindwa kwake
kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari na kuondoa
sheria kandamizi.
Imeandaliwa na Keneth M Mwandemange kwa msaada wa Gazeti la mwananchi
Imeandaliwa na Keneth M Mwandemange kwa msaada wa Gazeti la mwananchi
0 comments:
Post a Comment