KIKWETE ATAKAPONG'ATUKA,ATAKUMBUKWA KWA LIPI?
Ingawa aliingia madarakani kwa bashasha nyingi na
kauli mbiu zilizotia hamasa, lakini sasa anasema kazi ya urais ni ngumu
na anatamani amalize kipindi chake ili awe mtu huru.
Hotuba aliyotoa Rais Jakaya Kikwete, Oktoba 2014
alipokuwa Beijing, China ni kama alianza kuwaaga Watanzania akijiandaa
kustaafu urais.
Ingawa aliingia madarakani kwa bashasha nyingi na
kauli mbiu zilizotia hamasa, lakini sasa anasema kazi ya urais ni ngumu
na anatamani amalize kipindi chake ili awe mtu huru.
“Ni kweli naona kama muda hauendi kwa kasi ya
kutosha ili niweze kuwa raia wa kawaida na nipate muda wa kuchunga
ng’ombe na mbuzi wangu, nilime mananasi yangu kwa nafasi ya kutosha,”
alisema Rais Kikwete alipokuwa mkutanoni nchini China.
Kama ilivyo ada, kila anayemaliza ngwe yake huacha
kumbukumbu. Iwe mbaya au nzuri, swali ni je, yeye atakumbukwa kwa mambo
gani? Je, kuna watakaolia kwa furaha kuondoka kwake au watalia kwa
majonzi kwamba hawajui kesho yao?
Kikwete atakumbukwa kwa mambo makubwa na mazuri
aliyowafanyia Watanzania, lakini vile vile wapo watakaomkumbuka jinsi
alivyowaangusha kwa kutenda kinyume cha ahadi zake na kaulimbiu zake za
Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya au Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.
Watanzania wa kada mbalimbali wanazo sababu za
kumkumbuka Rais Kikwete atakapong’atuka madarakani. Hii itatokana na
jinsi walivyonufaika au kuumizwa kwa namna moja ama nyingine na utawala
wake.
Wanawake
Wanawake ni kati ya makundi katika jamii ambayo
kwa namna ya pekee watamkumbuka Rais Kikwete kwa jinsi alivyothamini
mchango wao na uwezo wao kiutendaji.
Ni katika awamu ya nne tangu ashike wadhifa huo,
alipoongeza kasi ya kuwaamini na akawateua kwa wingi baadhi yao kuingia
kwenye vyombo vya uamuzi kama uwaziri, ukuu wa mikoa na wilaya na nafasi
za uwakilishi kimataifa.
Katika kipindi chake, idadi ya majaji wanawake
iliongezeka, ikiwamo hata kufanikisha Anne Makinda kuwa mwanamke wa
kwanza kushika nafasi ya juu ya Spika wa Bunge. Je, atawaachia zawadi
wanawake kwa kupendekeza mmoja wao kuwa mgombea urais?
Vijana
Wazee
Wazanzibari
Wasomi
Wanachama wa CCM
Wakulima
Wananchi
Uchumi
Vyama vya upinzani:
Wanahabari
Vijana
Kundi hili nalo litakuwa na kila sababu ya kuhuzunika Kikwete
atakapoondoka madarakani. Hii ni kwa sababu kila alipofanya uteuzi,
hakuwaacha vijana.
Tangu alipojitosa katika kinyang’anyiro cha urais
kwa mara ya kwanza mwaka 1995, mkakati wake ulikuwa kuwapa vijana fursa
za uongozi na aliposhinda mwaka 2005 aliwateua bila hofu katika nyadhifa
mbalimbali.
Mifano ya vijana hawa ni kama January Makamba,
Lazaro Nyalandu, Mwigulu Nchemba (uwaziri); Lucy Mayenga, Halima
Dendegu, Wilmand Ndilu, Paul Makonda na wengineo (ukuu wa wilaya).
Wazee
Mbali na kuendelea kuamini busara za wazee, kila
alipotaka kutangaza jambo zito au kutoa hotuba ya mwisho wa mwezi
iliyotikisa nchi, alikutana na wazee ama Dar es Salaam au Dodoma, lakini
vile vile wazee wamo katika nafasi mbalimbali za uongozi; uwaziri, ukuu
wa wilaya na mikoa.
Wazanzibari
Rais Kikwete alijitahidi kadri ya uwezo wake kupatanisha wananchi wa Unguja na Pemba waliotofautiana kwa misingi ya siasa.
Chini ya ushawishi wake Wazanzibari walikubali
kuongoza nchi kwa ushirikiano; wakaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Uhasama uliondoka japokuwa kuna viashiria vya uhasama kurudi.
Wasomi
Hakuacha nyuma kundi la wasomi, kwani miongoni
mwao ndiyo wanaoongoza wizara nyeti na taasisi mbalimbali. Aliwateua
katika nafasi mbalimbali za uongozi japokuwa baadhi yao wamemwangusha.
Atakumbukwa alivyohamasisha ujenzi wa shule za
sekondari kukidhi ongezeko kubwa la wanaofaulu kutoka shule za msingi na
alivyojenga Chuo Kikuu cha Dodoma, upanuzi wa Chuo Kikuu Huria na vyuo
vya kati.
Wanachama wa CCM
Tofauti na vyama vingine vya siasa, CCM wanajivunia kumpata mtu
aliyekuwa kete ya ushindi kwa vipindi viwili mfululizo 2005—2010 na
2010—2015.
Watamkumbuka alivyowabeba, alivyofanyia
marekebisho katiba ya chama kuwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu kutoka
wilayani, alivyohuisha chama hadi kuwa na mvuto kuliko awali.
Hofu yao ni je, watampata mgombea ambaye atakuwa kete ya ushindi?
Wakulima
Kwa mara ya kwanza tangu Serikali ianze kuimba
wimbo wa kilimo ni uti wa mgongo, safari hii wakulima na wafugaji
walithaminiwa kiasi kwamba walipewa mbolea ya ruzuku, majosho na
alitatua migogoro ya ardhi na malisho japo kwa kasi ndogo.
Wananchi
Watamkumbuka alivyowapa vyandarua, alivyojenga
zahanati, vituo vya afya na alivyoongeza vifaa na majengo katika
hospitali kadhaa, hususan katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili;
vitengo vya upasuaji wa moyo na vinginevyo.
Kigoma watamfurahia alivyojenga daraja la Mto
Malagalasi pamoja na barabara ya kuunganisha na Mkoa wa Tabora; Kusini
watamkumbuka alivyokamilisha daraja la Umoja; alivyoongeza vivuko na
alivyofurukuta kukamilisha kipande cha kilomita 60 kutoka Ndundu hadi
Somanga katika barabara ya Dar es Salaam – Mtwara iliyoanza kujengwa
mwaka 1996.
Uchumi
Mabadiliko ya sheria ya uwekezaji angalau
yamewezesha nchi kuanza kunufaika na kodi ya uzalishaji, ingawa bado si
kwa kiasi kikubwa.
Ni katika utawala wa Rais Kikwete ambapo kumekuwa
na uboreshaji wa huduma za kibenki, mikopo ya saccos, uboreshaji wa njia
za uchukuzi kama barabara, vivuko, reli kwa kununua vichwa na mabehewa,
ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uwekezaji umeongezeka.
Vyama vya upinzani:
Miongoni mwa watakaolia kwa furaha ni wapinzani wakikumbuka
kiongozi huyo alivyoshindwa kujali haki za binadamu na ushahidi ni namna
Jeshi la Polisi lilivyotiririsha damu ya wapinzani wake kisiasa.
Mifano mingine ni alivyokimbilia kusuluhisha
mgogoro wa Kenya huku polisi wakilaza watu kwa risasi Mtwara kufuatia
mgogoro wa gesi; na Serikali yake ilivyoanzisha Operesheni Tokomeza
Ujangili iliyoishia kutiririsha damu ya watu wasio na hatia kama
wakulima, wafugaji na wawindaji lakini si majangili.
Wanahabari
Tasnia nzima ya habari kwa kiasi kikubwa,
itamkumbuka Rais Kikwete kwa jinsi Serikali yake ilivyonyonga uhuru wa
habari kwa kufungia magazeti kama Mwananchi, MwanaHalisi, Mtanzania,
Kulikoni na hivi karibuni The East African na zaidi askari polisi
walivyomuua mwanahabari Daudi Mwangosi chini ya utawala wake.
Kubwa zaidi kwa wanahabari ni kushindwa kwake
kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari na kuondoa
sheria kandamizi.
Imeandaliwa na Keneth M Mwandemange kwa msaada wa Gazeti la mwananchi
Imeandaliwa na Keneth M Mwandemange kwa msaada wa Gazeti la mwananchi
BAJETI YA MWISHO YA RAIS KIKWETE YAWASILISHWA
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
SERIKALI
imewasilisha mwelekeo wa bajeti kwa Kamati ya Bunge, ambayo inalenga
zaidi kupeleka umeme na huduma za maji vijijini, kumalizia miradi ambayo
haijakamilika na kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya Salum alisema wanaandaa bajeti ambayo itasaidia
kumaliza mambo yote waliyoahidi, ambayo yameainishwa kwenye Ilani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo serikali iliahidi wakati wa kampeni za
uchaguzi mkuu uliopita.
"Bajeti
ya mwaka 2015/16 ni ya kipekee. Ni mwaka wa uchaguzi, ni mwaka ambao
serikali ya Awamu ya Nne inamaliza muda wake na serikali mpya kuingia
madarakani. "Ni mwaka ambao Mkukuta na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya
Milenia ya miaka mitano inafikia tamati, Malengo ya Milenia ya mwaka
2015 yanafikia ukomo na pia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama
Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 unakamilika," alisema.
Vipaumbele vya bajeti
Akiwasilisha
mwelekeo wa bajeti hiyo kwa wabunge jijini Dar es Salaam jana, Mkuya
alisema bajeti ya mwaka huu imejikita zaidi kutathmini na kuangalia
changamoto kwenye sekta ya maji, nishati, rasilimaliwatu na kumalizia
miradi ambayo haijakamilika.
"Vipaumbele
kwenye bajeti hii vimejikita zaidi kwenye kuandaa awamu ya pili ya
Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano utakaoanza Juni mwaka 2016, na mkazo
zaidi ni kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini, kuimarisha
rasilimaliwatu na kugharamia uchaguzi mkuu," alisema Mkuya.
Akifafanua,
alisema katika mwelekeo huo wa Bajeti mpya ya mwaka 2015/16, jumla ya
Sh takribani trilioni 23 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika
matumizi ya maendeleo na ya kawaida.
Alisema
katika matumizi ya maendeleo,vipaumbele vitano ambavyo vimetajwa hapo
juu (maji, umeme, rasilimaliwatu, kumalizia miradi viporo na kugharamia
uchaguzi mkuu). Jumla ya fedha zilizotengwa ni Sh trilioni 5.8.
Mchanganuo
wake ni kwamba fedha za ndani ni Sh trilioni 4.3 na fedha za nje ni Sh
trilioni 1.4 ambazo kwa ujumla zitatumika kwenye utekelezaji wa
vipaumbele vilivyoainishwa na kumalizia miradi ambayo haikukamilika
kwenye bajeti iliyopita.
Katika
sekta ya nishati, kipaumbele kimewekwa katika kuendeleza miradi ya umeme
vijijini, ambapo hadi sasa wateja 2,602 wa vijijini kwenye mikoa ya
Simiyu, Singida, Kagera,Tanga, Ruvuma na Iringa, wameunganishiwa umeme.
Aidha,
katika sekta ya maji vijijini, tathmini ya bajeti iliyopita, inaonesha
kuwa jumla ya miradi ya maji vijijini, ilikuwa 123 iliyojengwa na
kukamilika na idadi hiyo imewanufaisha wananchi 463,750.
Katika
bajeti hii, mkazo umewekwa katika kukamilisha miradi ya maji vijijini
ambayo haijakamilika, ikiwemo miradi ya ujenzi wa mabwawa ya Kawa mkoani
Rukwa, Bwawa la Sasajila lililopo Dodoma na bwawa la Mwanjoro lililopo
Shinyanga pamoja na miradi mingine kwenye maeneo mengine vijijini.
Akizungumzia
suala la Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ambalo
ni moja ya vipaumbele katika bajeti hiyo mpya, Mkuya alisema bajeti
imejikita katika kugharamia uchaguzi huo ili ufanyike na kupata serikali
mpya itakayoendelea kutekeleza bajeti hii.
Mwelekeo wa bajeti
Akizungumzia
mwelekeo wa bajeti, Mkuya alisema Serikali imepanga kutumia Sh trilioni
22.48 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo katika bajeti ya
mwaka 2015/16 huku utegemezi wa fedha za kigeni ukipungua kutoka
asilimia 14.8 ya mwaka wa fedha uliopita hadi asilimia 8.4 kwa mwaka
ujao wa fedha.
Bajeti ya mwaka 2014/15 ilikuwa ni Sh trilioni 19.9, hivyo mwelekeo wa bajeti hiyo inakuwa na ongezeko kwa takribani asilimi 16.
Alisema
katika fedha hizo, sh trilioni 16.71 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya
kawaida, ikijumuisha Sh trilioni 6.61 kwa ajili ya mishahara ya
watumishi wa Serikali na taasisi, Sh trilioni 3.41 kwa ajili ya matumizi
mengineyo ya Wizara huku mikoa ikiwa ni Sh bilioni 83.55 na Mamlaka za
Serikali za Mitaa ni Sh bilioni 208.75 wakati Sh trilioni 2.60
zikitengwa kwa ajili ya kulipia hati fungani na dhamana za serikali
zinazoiva.
Aidha,
Mkuya alisema matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh trilioni 5.77 sawa na
asilimia 25.9 ya bajeti yote ambapo kiasi cha sh trilioni 4.33 ni fedha
za ndani sawa na asilimia 75 ya fedha za maendeleo na trilioni 1.44
fedha za nje.
"Kwa
kuzingatia sera za uchumi na misingi ya sera za bajeti, sura ya bajeti
inaonesha kuwa Sh trilioni 22.48 zinatarajia kukusanywa, ambapo mapato
ya ndani ya Serikali Kuu yanatarajia kuwa Sh trilioni 14.82 ambayo ni
sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote."
Alisema
serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 13.35
sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani huku mapato yasiyo ya kodi ni
Sh bilioni 949.2 na yale yatokanayo na vyanzo vya halmashauri
yanatarajia kuwa Sh bilioni 521.9.
Mkuya
alisema Serikali inategemea kukopa kiasi cha Sh trilioni 5.77 kutoka
vyanzo vyenye masharti ya kiabishara huku washirika wa maendeleo
wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 1.89 sawa na asilimia 8.4 ya bajeti,
ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/15 ambazo sehemu
kubwa ni mikopo ya masharti nafuu. CHANZO: HABARI LEO
BOTI YA TANZANIA YANASWA NA UNGA SCOTLAND
BOTI yenye usajili wa Tanzania,
imekamatwa kwenye Bahari ya Kaskazini na baada ya kupekuliwa katika
bandari ya Arberdeen huko Scotland, imekutwa na shehena ya dawa
zakulevya.
Kwa mujibu wa mtandao wa BBC, boti hiyo inayoitwa Hamal, yenye urefu wa mita 32 na uwezo wa kubeba tani 422, ilizuiwa Alhamisi na vyombo viwili vya ulinzi vinavyofanya doria ikiwa umbali wa maili 100 kutoka usawa wa bahari mashariki mwa mji wa Arberden.
Kwa mujibu wa mtandao unaoonyesha vilipo
vyombo vya baharini, katikati ya Februari, boti hiyo ilikuwa Uturuki na
wiki mbili zilizopita ilianza safari kutoka visiwa vya Tenerife
huko Hispania na ilipokamatwa ilikuwa inaelekea Hamburg, mji wa pili kwa
ukubwa wa Ujerumani ikitazamiwa kufika usiku wa Ijumaa iliyopita.
Boti hiyo imekutwa na watu 9 wenye umri
kati ya miaka 26 na 63 na wameshtakiwa kwa kukutwa na dawa za kulevya
wakitarajiwa kupelekwa mahakamani. Hata hivyo watu hao utaifa wao
haukuweza kupatikana mara moja.
John McGowan wa mamlaka inayoshughulikia
uhalifu kitengo cha ulinzi wa mipaka (NCA-BPC), amesema boti hiyo
imekamatwa na kiwango kikubwa cha dawa za kulevya na kukamatwa kwake
kumewezekana kutokana na ushirikiano wa taasisi za ulinzi za Uingereza
na ushiriiano wa kimataifa.
“Kiasi kamili cha dawa hizo bado
hakijafahamika na upekuaji bado unaendelea kwa ushirikiano wa NCA na
Jeshi la Polisi ya Scotland,” amesema.
Chanzo:Mwanahalisi Online
KAFULILA APATA TUZO YA KUFICHUA ESCROW
DAVID Kafulila-Mbunge wa Kigoma
Kusini (NCCR-Mageuzi), ametunukiwa tuzo na Mtandao wa Watetezi wa Haki
za Binadamu nchini (THRD), akiwa miongoni mwa watu watatu ambao
wamefanya kazi katika mazingira magumu kwa lengo la kutetea haki mwaka
2014.
Pamoja na Kafulila, wengine ni aliyekuwa
mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kundi la 201 akiwakilisha
Zanzibar, Salma Said na Mkurugenzi wa Baraza la Wanawake Wafugaji kutoka
Loliondo, Maanda Ngoitiko.
Akizungumza na MwanaHALISIOnline, Mratibu
wa THRD, Onesmo Ole Ngurumwa amesema watu hao ni wale “waliofanya kazi
ya kutetea haki za binadamu katika mazingira magumu huku wakitishiwa
kuuwawa lakini kazi zao zimesaidia kuleta mabadiliko”.
“Nawasihi watu waendelee kupigania haki.
Licha ya kwamba wanatishwa na hata wengine kuuwawa, wanapaswa kusimamia
kile wanachokiamini ambacho ni haki,” amesema Olengurumwa
Ameongeza kuwa, maaadhimisho haya ni ya pili kufanyika Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2013.
Ametaka siku hii itambuliwe kimataifa na isiwe nchini tu, huku
akisisitiza kwamba wanaofanya utetezi huo waangalie usalama wao katika
harakati za kupigania haki za wengine.
Naye Ernest
Sungura, Mkurugenzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF),
amesema katika kuelekea katika uchaguzi mkuu, wanahabari wanatakiwa
kulindwa na vyombo vinavyoweza kudhamiria kuwakingia kifua kutokana na
wao kuandika habari za uchunguzi ambazo mara kwa mara zimeonekana kugusa
maslahi ya watu mbalimbali moja kwa moja.
Wawakilishi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya nchini na washauri wa
masuala ya haki za binadamu katika nchi za Umoja wa Mataifa, wameeleza
kuwa, kama Serikali haithamini haki za mtu mmoja mmoja ipo hatari kubwa
ya kupoteza nguvu kazi ya taifa kwa jambo ambalo lingeweza kutatuliwa
kwa njia rahisi.Balozi wa Jumuiya ya Ulaya chini, Filberto Sebrregondi, amesema umefika wakati wa kila mwananchi kutambua kuwa wimbi la kuminywa haki za watu wasio na uwezo linakuwa kwa kasi nchini, licha ya kubainisha kwamba amefurahishwa kwa namna washiriki walivyoonyesha ushirikiano kwa mwamvuli wa mitandao hiyo ya kutetea haki za binadamu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo-Bisimba, akiongea katika maadhimisho hayo, alisisitiza kwamba haki za binadamu ndizo zinazowafanya wanadamu waishi na kwamba mtu yeyote asipofanya utetezi wa haki za binadamu anataka ubinadamu wa wengine uishie njia panda.
Kwa upande wake, Kafulia ambaye amepewa
tuzo hiyo kwa kuibua bungeni kashfa ya ufisadi wa Sh. 306 bilioni katika
akaunti ya Tegeta Escrow, ameliambia MwanaHALISIOnline kuwa “tuzo hii
imenipa ujasiri zaidi katika kusimamia maslahi ya taifa katika vita vya
ufisadi. Inaonesha katika mapambano haya sipo peke yangu”.
“Ni mara yangu ya kwanza kuingia bungeni.
Tena nikiwa kijana. Hakuna mbunge aliyewahi kukabidhiwa tuzo hii hasa
kwa kazi niliyoifanya ya kuibua ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow.
Inaonesha vijana tunaweza. Japo ilikuwa ni kazi hatari na wakati
mwingine nilitishiwa maisha yangu,” amesema Kafulila.
Ameupongeza mtanda wa THRD na Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa ushauri wa kisheria waliompa
wakati akitoa ushahidi wa ufisadi wake kwenye mamlaka za uchunguzi na
hata alipofunguliwa kesi na Seth Herbinder Singh, mmoja wa wanufaika wa
fedha za Escrow.
Naye Salma Said, alitishiwa maisha baada
ya kuonesha msimamo wake hadharani wa kupinga Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa akisema “ni kinyume na maoni yalitotolewa na wananchi”
huku Ngoitiko akiwa ni mtetezi wa haki za binadamu vijijini hasa
wafugaji walionyang’anywa maeneo yao Loliondo mkoani Arusha.
Tuzo hizo zimejumuisha cheti cha kutambua mchango wa kupigania haki na ngao ambayo ni alama ya ushujaa.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na
maonyesho ya watetezi hao, ambao ni Kampuni ya Jamii Media (Wamiliki wa
mitandao maarufu ya kijamii nchini ya FikraPevu.com na
JamiiForums, TGNP Mtandao, TAMWA, LHRC, HAKI ARDHI INSTITUTE, JUKWAA LA
KATIBA, TAWLA, SIKIKA, ZLSC, TAS, TACOSODE, TANLAP, LEAT,Human Rights
Comission, TVVA, Haki Catalyst, German Foundation, German Embasy, SANA,
na CESOPE.
293 WAOKOLEWA NCHINI NIGERIA KUTOKA KAMBI ZA BOKO HARAM
Jeshi
la Nigeria limesema limewaokoa watoto wa kike mia mbili na akina mama
tisini na tatu kutoka katika kambi ya Boko Haram iliyoko katika msitu wa
Sambisa, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Jeshi hilo limesema watoto
hao waliokolewa si kati ya wale waliotekwa mwaka mmoja uliopita na kundi
la kiislamu katika eneo la Chibok.
Jeshi limeiambia BBC kwamba
wanawake na watoto hao wa kike walikutwa katika kambi nne tofauti ambapo
silaha pia zimekamatwa,Msemaji wa jeshi amesema waliwapata wasichana
hao baada ya kuziharibu kambi hizo."ni muda mfupi tu uliopita, wanajeshi wetu wameingia katika msitu wa Sambisa, kutokea upande wa Alafa, ambapo walikuta kambi nne zinazomilikiwa na wapiganaji na kuziharibu, hapo ndipo walipogundua kuwa kuna wasichana wapatao mia mbili na wanawake tisini na tatu."
Kwa sasa jeshi limezuiwa kutoa utambulisho wa wasichana hao. Hata hivyo, jeshi limethibitisha kwamba wasichana hao sio wale wanafunzi waliotekwa katika mji wa Chibok.
"tuko katika mchakato wa kuwachunguza hawa wasichana ili tuweze kubaini utambulisho wao, lakini kitu kimoja nataka nikiweke wazi kwa umma, tunapotaja idadi ya wasichana mia mbili, tayari watu wanaanza kufikiria wasichana mia mbili wa Chibok waliotekwa mwaka jana, hawa sio wasichana wa Chibok, tutaendelea kuwajuza kadri muda unavyokwenda iwapo kutakuwa na taarifa zozote. "
Credit:BBC