Home » » ZEC yavitega vyama

ZEC yavitega vyama


Salum Kassim Ali, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC
Salum Kassim Ali, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeviandikia vyama 14 vya siasa vieleze msimamo wao kuhusu kushiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika 20 Machi 2016. Uchaguzi huo una maana ya kufuta kabisa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba ambao ulifutwa wote. 
Salum Kassim Ali, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, amethibitisha kuandika alichokiita muongozo kwa vyama vilivyoshiriki uchaguzi uliofutwa 28 Oktoba akitaka vitoe tamko la kuthibitisha kama vitashiriki uchaguzi wa marudio.
Salum amenukuliwa na gazeti moja akisema kwamba ameandika muongozo huo 25 Januari akitaka viwe vimetoa uhibitisho ifikapo tarehe 11 Februari.
Vyama hivyo 14 vilisimamisha mgombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi ambao siku tatu baada ya kuwa matokeo ya kura za urais yakiwa yanaendelea kutangazwa, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha aliitangaza akiwa katika udhibiti wa dola, kuufuta kwa madai kuwa umekumbwa na matatizo.
Wakati huo uchaguzi ukifutwa, Jecha alikuwa ameshatangaza matokeo ya majimbo 33 ya uchaguzi, majimbo tisa yakisubiri kutangazwa baada ya kukamilika kuhakikiwa kura zake na majimbo 12 yaliyobaki yakisubiri uhakiki.
Aidha, wakati Jecha akitangaza kufutwa kwa uchaguzi wote, tayari majimboni washindi wa uwakilishi na udiwani walishapatiwa hati zao za uthibitisho wa kushinda uchaguzi. Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Na.11 ya mwaka 1984, hati hizo hutolewa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo na malalamiko kuhusiana na matokeo yake yatafanyiwa kazi na mahakama tu.
Hata hivyo, Chama cha Wananchi (CUF) hakijapokea barua ya Mkurugenzi wa Uchaguzi kujulishwa kuhusu kutakiwa kuthibitisha kushiriki uchaguzi wa marudio.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Omar Ali Shehe, amesema mpaka jana, hawajapokea barua hiyo ya muongozo ingawa nao walishiriki kwa kuweka mgombea urais katika uchaguzi uliofutwa.
“Pamoja na kusema kuwa hatutashiriki uchaguzi wa marudio, tunapaswa kupatiwa mawasiliano yote yanayotoka Tume kwa kuwa ni haki yetu kujua kila kinachoendelea ndani ya tume,” alisema Shehe ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) la CUF.
Vyama vilivyopata barua ya ZEC ni ACT-Wazalendo kilichomsimamisha Khamis Iddi Lila, TADEA kilichomsimamisha Juma Ali Khatib, ADC alichoteuliwa Hamad Rashid Mohamed, AFP alichoteuliwa Said Soud Said, CCK alichoteuliwa Ali Khatib Ali, Chauma alichoteuliwa Mohamed Masoud Rashid.
Vingine ni Demokrasia Makini alichoteuliwa Tabu Mussa Juma, DP alichoteuliwa Abdalla Kombo Khamis, Jahazi Asilia alichoteuliwa Kassim Bakari Ali, NRA alichoteuliwa Seif Ali Iddi, SAU alichoteuliwa Issa Mohamed Zonga, CCM alichoteuliwa Dk. Ali Mohamed Shein na TLP alichoteuliwa Hafidh Hassan Suleiman.
Tayari baadhi ya vyama vimeshatangaza kuwa havitashiriki uchaguzi wa marudio, vingine vikiwa vinaendelea kujadiliana.
CUF kilishasema hakitashiriki uchaguzi huo kwa msimamo kuwa hakukuwa na uhalali wa kisheria wa kufutwa uchaguzi mkuu kwa vile Tume haikuwa na mamlaka ya kufanya hivyo. Chama hicho kinashikilia kuitaka Tume ikamilishe kazi ya kutangaza matokeo ya kura za majimbo yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa urais.
Kinasema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki lakini CCM ilikula njama na vyombo vya dola na kumshinikiza Jecha aufute uchaguzi huo baada ya kubaini kilishindwa.
Toa maoni yako kwa habari hii kwa kuweka email yako hapa,na endelea kutufatilia zaidi Ukurasa wa habari

0 comments:

 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger