WATU
watano wa familia moja wakiwemo wanafunzi wanne wamekufa papo hapo kwa
kupigwa radi wakiwa shambani katika Kijiji cha Manungu kata ya Uyogo,
Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya
Kahama, Leonard Nyadaho, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Shinyanga, watu hao walipigwa na radi Februari 28, mwaka huu na kufariki
papo hapo kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.
Nyadaho
alisema mvua hiyo iliyoanza kunyesha juzi jioni katika kijiji cha
Manungu kitongoji cha Izengwe. Alisema mvua hiyo iliwakuta wananchi hao
wakiwa mbugani wakipanda mpunga ndipo walipopigwa na radi na kufariki.
Aliwataja
marehemu hao kuwa ni Paulina Williamu (28), Magreth Mayunga (13),
Herena Mayunga (14), Flora Mathias (13) na Veronica Mathias (14), wote
wanafunzi wa Shule ya Msingi Manungu.
Mashuhuda
walisema marehemu hao waliamka asubuhi na kwenda shambani kupanda
mpunga, wakiwa huko ghafla lilitanda wingu zito ndipo mvua iliyoambatana
na radi ilipoanza kunyesha.
Walisema
mvua hiyo kubwa iliyokuwa imeambatana na upepo mkali ilikuwa na
muungurumo wa radi wa mara kwa mara. Walisema ilinyesha muda mfupi na
ilipokatika walisikia mayowe yakitokea walipokuwa watu hao.
"Baada ya kwenda shambani tulikuta wote hao wameshafariki," alisema mmoja wa mashuhuda hao.
0 comments:
Post a Comment