Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Siku moja baada ya katibu mkuu wa
Chadema, Dk Willbrod Slaa kuwataka Watanzania wajiandae kwa “Serikali
Mpya” aliyodai itapatikana Oktoba 31 baada ya Uchaguzi Mkuu, gazeti la
Mwananchi limebaini mkakati wa ushindi unaopangwa na chama hicho cha
upinzani.
Hadi sasa, Chadema ndio chama kinachoongoza kwa
upande wa upinzani kulingana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita na wa
Serikali za Mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, na inaonekana
kujipanga kupaka mafanikio makubwa zaidi mwezi Oktoba.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, mgombea wa CCM,
Jakaya Kikwete alishinda kwa kupata asilimia 61.17, ikiwa ni pungufu ya
asilimia 20 ya kura alizopata mwaka 2005, wakati Chadema ilimsimamisha
Dk Willbroad Slaa aliyepata asilimia 26.34 akiwa anasimama kwa mara ya
kwanza.
Huku CCM ikiwa katika mchakato mgumu wa kumpata
mrithi wa Kikwete uliogubikwa na adhabu dhidi ya makada wanaotajwa
kutaka nafasi hiyo, Chadema iliweka mkakati wake katika kikao cha Kamati
Kuu kilichofanyika Januari mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari ambazo Mwananchi imezipata,
chama hicho kimelenga pamoja na mambo mengine kupeleka madaraka kwenye
ngazi ya kanda badala ya mambo yote kutegemewa yafanywe na makao makuu.
Chadema, habari hizo zinasema, imeunda kanda 10
ambazo ni Kanda ya Serengeti, inayoundwa na mikoa ya Simiyu, Shinyanga
na Mara, Ziwa Victoria (Geita, Mwanza, Kagera), Nyanda za Juu Kusini
(Rukwa, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Iringa), Kanda ya Kusini (Lindi na
Mtwara).
Nyingine ni Kanda ya Kati (Singida, Dodoma na
Morogoro), Kanda ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara),
Kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Kanda ya Pwani (Temeke,
Ilala na Kinondoni), Kanda ya Unguja(Kusini Unguja, Kaskazini Unguja na
Mjini ) na Kanda ya Pemba (Kusini Pemba na Kaskazini Pemba).
Kanda hizo zitawezeshwa kwa mafunzo na kiuchumi
ili kuzijengea uwezo wa kushughulikia mambo yake, hasa wakati wa
uchaguzi bila ya kutegemea ofisi kuu.
Kwa mujibu wa habari hizo, kanda hizo pia
zinazindua vikundi vyake vya ulinzi, ambavyo kazi kubwa inaonekana
itakuwa ya kulinda kura ili kukabiliana na tatizo kubwa la upungufu wa
rasilimali watu wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Pia kuundwa kwa Mabaraza ya Uongozi ya Kanda
kutawezesha mashauri mengi kwenye ngazi ya mikoa kutatuliwa bila ya
kutegemea ofisi kuu.
Tayari mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe
ameshafanya ziara kwenye baadhi ya kanda na kufanya vikao na Mabaraza ya
Uongozi ya Kanda kuyashirikisha mikakati hiyo, sambamba na kuzindua
vikundi vya ulinzi.
Lakini alipoulizwa kuhusu mpango huo, Mbowe hakutaka kuwa bayana.
“Sasa nikiweka wazi mikakati yetu, si itakuwa
kama nimewauzia wengine. Hapana siwezi kuiweka wazi ila tunajipanga
kuelekea Uchaguzi Mkuu,” alisema Mbowe, ambaye pia aligombea urais mwaka
2005 wakati Kikwete akiingia Ikulu kwa mara ya kwanza.
Lakini mtu aliye karibu na uongozi huo wa Chadema alikiri kuwapo kwa mkakati huo.
“Unajua mkakati huo unakwenda sambamba na kutoa
mafunzo kwa viongozi mbalimbali wa chama kuanzia ngazi ya chini kabisa,”
alisema akiomba jina lake lisitiriwe.
“Tunataka kanda hizi ziwe na uwezo wa kupambana na
si kusubiri kila jambo kutoka makao makuu.” Taarifa zaidi zinaeleza
kuwa ziara hizo za Mbowe pia zinalenga kufanya maboresho ya kiutendaji
ikiwa ni pamoja na viongozi wa chama hicho kupewa mafunzo maalum na
mbinu mbalimbali. “Chama kimebaini kuwa ili kushinda, hakiwezi kupambana
na adui kutoka sehemu moja tu, ni lazima kiwe nchi nzima.
Hilo tumeliona katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa,” alisema mtoaji habari huyo. “Kinachofanywa sasa ni kuhakikisha
kuwa kila kanda inakuwa na nguvu ya kufanya mambo yake yenyewe.
Yaani kila kanda itaweka mkakati wake wa
kukiimarisha chama na kukabiliana na misukosuko yote ya kisiasa. Makao
makuu ya chama yatakuwa yakitoa maelekezo tu.” Jumamosi iliyopita, Dk
Slaa alisema katika mkutano wa hadhara uliofanyika Isaka wilayani Kahama
kuwa nchi haina budi kujiandaa kwa serikali mpya.
Alisema Chadema itashika nchi kwa kuwa wananchi
wamechoshwa na serikali iliyopo sasa ya CCM, kwamba ili kuongeza nguvu
za kuking’oa chama hicho kikongwe, wananchi wanapaswa kuunga mkono
juhudi za Ukawa.
Dk Slaa, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Karatu
kabla ya kugombea urais mwaka 2010, anatazamiwa kuteuliwa tena na chama
chake kuwania urais na ni mmoja wa watu wanaopewa nafasi kubwa ya
kupitishwa na Ukawa kupeperusha bendera ya upinzani dhidi ya mgombea wa
CCM, kwenye mbio za Ikulu.
Mbali na kufanya vizuri mwaka 2010, Chadema
ilipiga hatua kubwa zaidi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana baada ya kunyakua viti vingi
vilivyokuwa vinashikiliwa na CCM na vyama vingine vya upinzani.
Chadema ilifanya vyema zaidi katika Kanda ya
Serengeti kwa kupata kura nyingi katika vijiji, vitongoji na mitaa, kura
ambazo hazijafikiwa na kanda yoyote.
Kanda nyingine zilizofuatia kwa kufanya vizuri katika uchaguzi huo ni Kanda ya Ziwa Victoria na Kanda za Kaskazini.
CHANZO;MWANANCHI
CHANZO;MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment