Wanamgambo
wa kundi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria wamewateka nyara
wanawake na watoto mia nne katika shambulio walilofanya mapema mwezi huu
kwenye mji wa Damasak ulioko kilomita kadhaa kutoka kwenye mpaka wa
pamoja wa nchi hiyo na Chad. Mji huo wa kaskazini mashariki mwa Nigeria
uliokuwa ukishikiliwa na kundi la Boko Haram ulikombolewa na jeshi la
nchi hiyo siku kumi zilizopita. Kwa mujibu wa mashuhuda, wanamgambo wa
kundi la Boko Haram waliwaua watu 50 miongoni mwa mateka hao kabla ya
kurejea nyuma kwenye ngome zao. Hadi sasa hakuna taarifa za uhakika
kuhusu hatima ya mateka waliosalia. Tangu kundi la kigaidi la Boko Haram
lilipoanzisha mashambulio yake ndani ya ardhi ya Nigeria mwaka 2009,
makumi ya maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni moja
wamelazimika kuyahama makaazi yao. Kutokana na kuendelea mashambulio ya
kundi hilo katika miaka ya hivi karibuni, na kushindwa jeshi la Nigeria
kukabiliana na mashambulio hayo, hatimaye mnamo tarehe 14 ya mwezi
uliopita wa Februari, Nigeria yenyewe pamoja na Chad na Niger
zilianzisha operesheni za pamoja za mashambulio dhidi ya Boko Haram.
Muungano huo wa kieneo uliongeza matumaini ya kulitokomeza kundi hilo la
kigaidi. Viongozi wa Nigeria wametangaza hivi karibuni kuwa miji 38 ya
kaskazini mashariki imekombolewa, na magaidi wa Boko Haram wametimuliwa
kutoka kwenye majimbo kadhaa waliyokuwa wakiyashikilia hususan jimbo la
Borno. Huku ripoti zikieleza kuhusu kufurushwa na kurudi nyuma kundi la
Boko Haram
kutoka
maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na kundi hilo, kutangazwa ghafla habari
ya kutekwa nyara idadi kubwa ya wanawake na watoto kumewatia hofu na
mshtuko wananchi wa Nigeria. Kuibuka tena habari za shambulio na utekaji
nyara uliofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram kumejiri wakati siku
chache nyuma Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria alikuwa ametangaza
kwamba kundi hilo litakuwa limekwisha sambaratishwa ndani ya kipindi cha
mwezi mmoja. Akizungumza kwa matumaini makubwa alisema hautopindukia
muda wa mwezi mmoja kabla ya Boko Haram kutimuliwa na kutolewa nje ya
ardhi ya Nigeria. Rais wa Nigeria alitilia nguvu madai yake hayo kwa
kuashiria kukombolewa vijiji na maeneo kadhaa katika kipindi cha wiki
zilizopita kwa msaada wa majeshi ya nchi jirani, yaani Chad, Cameroon,
Niger na Benin. Kwa muda mrefu, wananchi wa Nigeria wamekuwa
wakimshutumu kiongozi wao huyo kwamba anaonyesha ulegevu katika
kukabiliana na kundi la Boko Haram. Bali kuna hata wale waliokwenda
mbali zaidi kwa kutamka kwamba Rais Jonathan anawaunga mkono nyuma ya
pazia magaidi hao. Wapinzani wa serikali wanaeleza kwamba Jonathan
analiunga mkono kwa siri kundi la kigaidi la Boko Haram kwa shabaha ya
kuwadhoofisha Waislamu. Lakini madai yote hayo ya wapinzani yanapingwa
na waungaji mkono wa kiongozi huyo. Itakumbukwa kuwa mnamo siku kadhaa
nyuma, kwa mara ya kwanza, Rais wa Nigeria alikiri kwamba serikali yake
haikuichukulia kwa uzito unaostahiki hatari ya kundi la Boko Haram na
hivyo kuandaa suhula chache kwa ajili ya kupambana na kundi hilo. Kwa
mtazamo wa wataalamu wa mambo tukio la kutekwa nyara idadi kubwa ya
wanawake na watoto litaathiri nafasi ya Rais Jonathan katika uchaguzi
mkuu ujao wa Nigeria. (CHANZO:Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran)
0 comments:
Post a Comment