PAUL NONGA AMFUATA JULIO.....AJIFUNGA MWAKA MMOJA MWADUI FC

      

 

Klabu ya Mwadui ya mkoani Shinyanga imefanikiwa kumsajili mshambuliaji Paul Nonga kutoka katika klabu ya Mbeya City kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Nonga ametua katika klabu hiyo iliyopanda daraja msimu huu kufuatia mkataba wake katika klabu ya Mbeya City kumalizika.

Akiongea na Ukurasa Wa Habari kutokea moja kwa moja mkoani Shinyanga mchana huu, Nonga amesema kikubwa zaidi ni kutafuta changamoto mpya na upande wa masirahi pia mwadui wapo vizuri. "Mimi nimefurahi kurudi nyumbani ,hii ni changamoto mpya na kingine kilichonishawishi kuja hapa ni masuala ya masirahi ,mwadui wapo vizuri "amesema Nonga

Mshambuliaji huyo ni moja ya wachezaji waanzilishi wa Mwadui Fc,aliichezea timu hiyo miaka ya nyuma wakati wanatafuta nafasi ya kupanda ligi daraja la kwanza lakini wakashindwa baada ya Rhino Rangers kuwapiku.

Baada ya hapo Nonga alihamia jkt Oljoro na baadaye Mbeya City ambapo amecheza kwa misimu miwili huku akiwa mshambuliaji tegemezi wa timu hiyo ya jijini Mbeya

Mwadui iliyopo chini ya kocha mwenye maneno mengi Jamhuri Julio Kihwelu itacheza katika ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu ujao mara baada ya kufanikiwa kupanda daraja msimu huu kuingia kunako ligi hiyo.

                                                         

MISWADA HII YA HABARI NI KITANZI KINGINE KWA CCM

 Reginald Mengi
 Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu mswada wa sheria ya vyombo vya habari ambao ulitaka kuwasilishwa bungeni kwa dharula.
 Mwenyekiti wa MOAT Reginald Mengi

Ukweli ni kuwa kila binadamu ana haki ya kupata maendeleo anayoyahitaji, ili kukuza na kustawisha utu wake.

Uhuru wa habari ni kati ya haki muhimu za binadamu ambazo zinatambuliwa na dunia nzima kikatiba. Watu wa habari tunaamini kwamba ‘hakuna maendeleo bila habari.’

Ukweli ni kuwa kila binadamu ana haki ya kupata maendeleo anayoyahitaji, ili kukuza na kustawisha utu wake.

Mungu alimuumba mwanadamu kwa uhuru na matakwa yake, hivyo Mungu anamshirikisha mwanadamu uhuru huo ili amtambue, amtumikie, amsifu na kumwabudu.

Kwa hivyo, kukosekana au kuminywa kwa uhuru wowote ule, uwe wa kisiasa, wa uchumi wa kuabudu (dini), kifkra, kiutamaduni na hasa uhuru wa habari, ni kuwafanya watu kuwa wendawazimu.

Kama kuna kitu mwanadamu yeyote anakipigania kwa akili zote na nguvu zote, basi ni uhuru ambao ni haki ya msingi ya kila mwanadamu.

Katiba Inayopendekezwa inasema: “ Kila mtu ana haki na uhuru wa kutafuta, kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa sahihi.

Ibara hiyo inaendelea kusema kwamba kila mtu ana uhuru wa kuanzisha vyombo vya habari na njia nyingine za upashanaji habari.

Miswada ya habari

Wakati ibara hiyo imewekwa vizuri katika katiba hiyo, miswada miwili inayokaribia kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete inabomoa uhalisia huu.

Muswada umetengeneza mazingira magumu ya upatikanaji wa habari pamoja na usambazaji wake.

Mimi kama mwanahabari, najiuliza hivi Serikali yetu ina malengo gani na tasnia ya habari? Je, ina lengo la kuboresha au kukandamiza uhuru wa habari hasa kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu?

Nikiwa nchini Ghana, niliwahi kusoma habari za malalamiko mengi kuhusiana na miswada hii miwili ya habari.
Muswada mmoja unahusu upatikanaji wa habari na wa pili unahusu usimamizi wa vyombo vya habari. Ni kweli uhuru bila mipaka pia ni uwendawazimu.
Viongozi wa dini
Gazeti moja la kila siku lilieleza habari za viongozi wa dini hususani maaskofu wa Kanisa Katoliki na Baraza la Waislamu waliokutana, ili kujadili kadhia hiyo inayohusu uhuru wa habari nchini katika dunia hii ya ukuaji wa tasnia ya habari.
Kabla ya viongozi hawa wa dini kukutana na kujadiliana kero hii, tayari wabunge hasa wale wa upinzani walishatoa kauli zao za kutokubaliana na sheria hizo ambazo zinalenga kukandamiza uhuru wa habari nchini, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015.
Viongozi hao wanatamka wazi kwamba iwapo miswada hiyo itaisainiwa na Rais, nchi hii itageuka ya kidikteta kama enzi za mkoloni.
Kwa kawaida, ukiona viongozi wa dini ambao ni wasomi, wenye busara na wanaoongozwa na uchaMungu wanakutana kujadili masuala ya jamii, ujue kwamba jambo hilo Serikali imepoteza mwelekeo.
Kwa mfano, viongozi wa dini walionya mapema juu ya upungufu katika mchakato wa katiba mpya, lakini Serikali ikapuuzia; na leo matokeo yake kura ya maoni imesitishwa.
Gharama zilizotumika katika mchakato huo ni kubwa kupindukia. Wahenga wanasema: ‘asiyesikia la mkuu huvunjika guu.’
Wadau wengine wa habari wameshatoa maoni yao na kuitaka Serikali kurekebisha upungufu uliomo katika miswada hii ya habari, lakini hata hivyo Serikali inaonekana kushikilia msimamo wake.
Wamiliki wa vyombo vya habari nchini chini ya uenyekiti wa Reginad Mengi nao wametoa maoni yao na hofu yao juu, lakini je, Serikali itasikiliza vilio vya wadau hao?
Baadhi ya sheria zilizomo katika miswada hiyo hakika ni kinyume kabisa cha ukuzaji wa uhuru wa habari.
Kwa mfano, kuwadai waandishi wa habari kuwa na digrii ya kwanza kama kigezo cha kuwa mwandishi wa habari, ni kuikandamiza habari.
Je, ni kwa nini digrii ianze na waandishi na si wabunge, mawaziri au madiwani? Wakati Serikali ikiweka masharti magumu kwa waandishi wa habari, inasemekena sifa ya mtu kugombea ubunge ni kujua kusoma na kuandika.
Kibaya zaidi sheria hizi kwa nini zilingoja hadi kipindi hiki cha mwisho cha uongozi wa awamu ya nne tena kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu? Je, wananchi wapate picha gani kuhusu sheria kandamizi kama hizi?
Tafsiri ya wananchi wengi ni kwamba Serikali imeshikwa pabaya katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, ndiyo kwa maana inakuja na sheria kandamizi kwa uhuru wa habari ili kuwanyima wananchi habari sahihi kuhusiana na uchaguzi huo.
Je, huku ndiyo kukua kwa demokrasia na utawala bora nchini Tanzania, kama tunavyojigamba katika medani za kisiasa?
Kwa upande mwingine, kama yalivyo masuala mengine ambayo yameleta migogoro katika jamii, hili nalo limeongeza mgogoro mwingine kwa serikali pamoja na wadau wa habari, wanahabari na pia viongozi wa dini.
Hivi nikisema miswada hii ni kitanzi kingine cha serikali ya CCM nitakuwa nimekosea? Je, viongozi wa dini wakiingilia kati watakuwa wameiingilia Serikali katika utendaji wake?
Viongozi wa dini wanashuhudia kwamba pole pole uhuru wa habari unapotea katika jamii yetu kwa masilahi binafsi ya wanasiasa wachache. Madhehebu ya dini yanamiliki pia vyombo vya habari, navyo vikubali kukandamizwa? Namuomba Rais Kikwete kutafakari kwa kina madhara ya kusaini miswada hii. Akumbuke kuwa hata chama chake hakiwezi kupona sheria hii ikipita.

Chanzo;MWANANCHI

UKAWA WAWAPONDA WALIOTANGAZA NIA CCM

 

 
 



Wafuasi wa Chadema wa mjini Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, wakiwa katika maandamano   ya kumsindikiza Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, Dk Wilbroad Slaa baada ya kumaliza kuhutubia  mkutano uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua mkoani humo. Picha na Godfrey Kahango 



    Washangaa makada kutumia fedha nyingi kwa kazi ndogo ya kutangaza nia


Sumbawanga/Dar. Viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wameponda tabia ya makada wa CCM wanaotangaza nia ya kugombea urais kufanya hafla zinazotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo.

Viongozi hao wamesema vitendo hivyo vinaonyesha kuwa chama hicho tawala hakichukii ufisadi na hivyo hakiwezi kuwa na mgombea safi.

Makada hao wamelipia muda wa matangazo ya moja kwa moja kwenye vituo vya redio na televisheni, kufanya maandalilizi ya gharama kubwa kwenye sehemu walizotangazia nia, kuandaa vipeperushi na mabango ya thamani huku baadhi wakituhumiwa kusafirisha watu kutoka sehemu mbalimbali kuhudhuria hafla hizo.

Akihutubia wakazi wa Sumbawanga mkoani Rukwa, katibu mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa alisema Serikali ya CCM ni kama ya watu wa ukoo mmoja wenye tabia zinazofanana.

Alisema Serikali imejaa tuhuma nyingi za rushwa na ufisadi na kwamba, kinachotakiwa ni kuinyima kura zote wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Katibu huyo alisema wale wote wanaojitokeza kutangaza nia ni ‘mafisadi’ ndio maana wanatumia nguvu ya fedha kuwanunua Watanzania, jambo ambalo alisema ni kinyume cha maadili.

“Ni hatari sana kuwachagua viongozi kwa fedha, hawa wanataka kuliangamiza Taifa,” alisema.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema anashangaa chama kilichoasisiwa na mjamaa Mwalimu Julius Nyerere, vijana wake wanafanya sherehe kubwa kwenye jambo dogo.

“Hata mwanasiasa mkongwe Kingunge (ngombare Mwiru) anakwenda kuwa mpambe kwenye shughuli inayokiuka taratibu,” alisema na kuongeza kuwa hiyo ni ishara mbaya.

Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi alihoji wanaotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo, watazirudishaje.

Alisema kama makada hao walifanya kazi halali, hawawezi kuwa na fedha zinazoweza kugharimia sherehe kubwa kama hizo.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mfumo mbaya wa CCM ndio unaonyesha chama hicho hakichukii mafisadi.

“Kama chama kingekuwa kinachukia ufisadi, kingeandaa utaratibu wake ili watu wote wanaotangaza nia wawe na nguvu sawa,” alisema Mbatia.

USAJILI; SIMBA YAWEWESEKA KWA MESSI

          
                 



Akizungumza kwenye makao makuu ya klabu hiyo, Msimbazi jijini Dar es Salaam, ofisa habari wa Simba, Haji Manara alisema klabu yao imeamua kumwaga mboga baada ya kuona inafanyiwa hujuma.


Dar es Salaam. Kimya kingi kina mshindo! Ndicho unachoweza kusema baada ya uongozi wa Simba kuibuka na kueleza kuwa utaishtaki Azam FC kutokana na kumshawishi kwa lengo la kumsajili Ramadhani Singano ‘Messi’ pamoja na kuponda usajili uliofanywa na wapinzani wao kwa Malimi Busungu.

Akizungumza kwenye makao makuu ya klabu hiyo, Msimbazi jijini Dar es Salaam, ofisa habari wa Simba, Haji Manara alisema klabu yao imeamua kumwaga mboga baada ya kuona inafanyiwa hujuma.

“Sisi Simba, sasa imetosha, kama watu wanaamua kumwaga ugali, sisi tunamwaga mboga, hatutaki kuyumbishwa,” alisema Manara kwa jazba huku akieleza kuwa muda wa kuyumbishwa kwa klabu yao umepita.

Hivi karibuni, Messi alihusishwa na kufanya mazungumzo ya kujiunga na Azam.

Kuhusu hilo, Manara alisema wanatafuta ushahidi ili kuishtaki klabu pinzani ambayo ilifanya mazungumzo na mchezaji huyo.

“Tumesikia kuna klabu imefanya mazungumzo na mchezaji wetu, Messi ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja, kama inamtaka ije tuipe dau letu, lakini si kuitana kinyemela.

Akijibu shutuma hizo, Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba alikanusha madai ya kufanya mazungumzo na Messi na kueleza kuwa haina mpango wa kumsajili nyota huyo wa Simba.

Sababu za kumkosa Busungu

Simba katika mchakato wa kupata saini ya mshambuliaji Malimi Busungu wa Mgambo JKT aliyejiunga na Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita na kumkosa.

Hata hivyo, Manara alibainisha kuwa ilimwacha nyota huyo ambaye alitaka fedha ambazo haziendani na thamani ya kiwango chake uwanjani.

“Tulimwambia ukweli Busungu kuwa kama ana nia ya kucheza Simba, dau letu ni Sh5 milioni, yeye akahitaji Sh40 milioni, fedha ambazo tulimwambia hatuwezi kumpa kwani hajafikia kiwango hicho,” alisema Manara.

Naye mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Simba, Zacharia Hanspoppe aliwaponda Yanga kiaina baada ya kudai kuwa wao hawataki kusajili wachezaji wanaovuma, bali wanasajili kwa kuangalia mahitaji ya timu.

Alisema anajua kuwa wengi wanataka kuona Simba ikisajili wachezaji wenye majina makubwa na wanaovuma hivi sasa, lakini wao hawaangalii hilo, wanachoangalia ni ubora wa mchezaji na mahitaji ya kikosi chao kwanza.
“Sisi wala hatutaki kushindana na mtu katika kusajili, eti huyu kasajili huyu na sisi tusajili yule, hilo kwetu halipo, tunachofanya ni kusajili kulingana na timu inahitaji nini kwa wakati huo,” alisema Hanspoppe.
“Timu yetu bado ni nzuri, inakosa mambo madogo madogo, hivyo tunachofanya ni kukiongezea nguvu katika nafasi ambazo tumeona zimepwaya na wala hatutaki kusajili mchezaji kwa sababu jina lake linavuma, tunasajili mchezaji tunayemhitaji na siyo anayevuma,” alisema Hanspoppe.
Rage ahusishwa sakata la Messi
Klabu ya Simba imekuwa katika marumbano na mshambuliaji wake, Ramadhan Singano ‘Messi’ ambaye anadai kughushiwa kwa mkataba wake. “Mkataba wa Messi tumeurithi kwa uongozi uliopita (mwenyekiti alikuwa Ismail Aden Rage) na walimsajili kwa mkataba wa miaka mitatu, leo hii anadai alisaini miaka miwili. “Dole gumba na saini ni ya Messi na tulipomuuliza alisema alisainishwa na Mzee Kinesi (Joseph Itang’are), niweke wazi kuwa Simba haijawahi na haiwezi kughushi mikataba ya mchezaji yeyote,” alisema.
Alisema klabu hiyo imeunda kamati maalumu kuchunguza jambo hilo na itachukua hatua stahiki baada ya uchunguzi wao kukamilika.
Yamtupia virago Amri Kiemba
Akizungumzia usajili wa mchezaji Amri Kiemba ambaye Azam aliyokuwa akiichezea kwa mkopo imeeleza dhamira ya kumrudisha ilikomtoa (Simba), Manara alisema klabu hiyo haina mpango na mchezaji huyo.
“Hatuna mpango wa kumrudisha Kiemba, hatuna nafasi hiyo,” alisema Manara ambaye hakuwa tayari kuweka wazi kama mkataba wa mchezaji huyo na klabu hiyo umemalizika au la.
Madeni yanayoikabili klabu
“Nakiri ni kweli tunadaiwa, lakini hakuna taasisi duniani ambayo haidaiwi, hata Marekani, nchi tajiri inadaiwa, sembuse Simba, tunajipanga ili kulipa madeni hayo,” alisema Manara.
Alikiri kuwa klabu yao inadaiwa na baadhi ya wachezaji wake iliyovunja nao mikataba, Amissi Tambwe na Donald Mosoti.

Ujio wa kocha mpya na usajili
Akizungumzia kazi ya usajili na kocha mpya, Manara alisema, kocha mpya atatangazwa ndani ya siku nne kuanzia jana baada ya uongozi kukamilisha mchujo wa makocha walioomba kuinoa timu hiyo.
“Usajili tunaendelea vizuri, na kweli nilikwenda kwenye mashindano ya Cosafa (Afrika Kusini) ili kuangalia wachezaji, mchakato utakapokamilika kila kitu kitawekwa wazi, tutasajili kutokana na mahitaji yetu msimu ujao na upungufu tuliokuwa nao msimu uliopita ,” alisema.

Iyanya x Diamond - Nakupenda [Official Video]

BLATTER AJIUZULU WADHIFA WAKE FIFA

 
Sepp Blatter ameliongoza Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kwa kipindi cha miaka 17.
Sepp Blatter ameliongoza Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kwa kipindi cha miaka 17.

Sepp Blatter, raia wa Uswisi, ambaye alichaguliwa kwa muhula wa tano Mei 29 kuliongoza Shirikisho la Soka Duniani Fifa, ametangaza katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne Mei 2 katika mji wa Zurich kwamba amejiuzulu kwenye wadhifa wake.
Uamzi huu unakuja kufuatia kashfa ya rushwa inayolikabili Shirikisho la Soka Dunia Fifa tangu Mei 27.
Akiwa ni mwenyekiti wa Fifa tangu mwaka 1998, Sepp Blatter ametangaza kujiuzulu Jumanne wiki hii katika mji wa Zurich, siku tano baada ya kuchaguliwa kwa muhula wa tano kama mwenyekiti wa Shirikisho hilo la kandanda Duniani.(P.T)
“ Nataka kuitisha mkutano wa dharura na kukabidhi muhula wangu kwa yoyote yule atakayeshinda katika kinyanga'nyiro cha kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Fifa”, amesema Blatter.
Sepp Blatter na timu yake wanatuhumiwa kutoa kiholela masoko ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi na Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.
“ Hata kama nilichaguliwa, sikupata uungwaji mkono wa pande zote ”, amesema Blatter katika mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Fifa.
Sepp Blatter, mwenye umri wa miaka 79, amekua akishikilia wadhifa huo tangu mwaka 1998. Mswisi huyo amebaini kwamba ataitisha mkutano wa dharura kati ya mwezi Desemba mwaka 2015 na Machi mwaka 2016.
“ Ntaendelea kushikilia wadhifa wangu kwa muda wa miezi kadhaa, kabla ya kumkabidhi mwenyekiti mpya atakaye kuwa amechaguliwa", ameongeza Joseph Sepp Blatter.
Ni uamzi mzuri, kwa mujibu wa Michel Platini
Rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa), Michel Platini, amekaribisha uamzi huo wa Sepp Blatter. Lakini baadhi ya marais wa mashirikisho ya Soka kutoka mataifa ya Afrika wameshtushwa na uamzi huo, hasa Constant Omari, rais wa shirikisho la Soka la Congo, ambaye amemsifu Sepp Blatter kuwa ni mtu jasiri na mwenye uamzi.
 Na RFI

17 MAHAKAMANI KWA JARIOBIO LA KUMPINDUA NKURUNZIZA



 

 
Bujumbura, Burundi. Maofisa 17 wa Jeshi la Burundi wametiwa mbaroni wakiwamo majenerali watano na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuipindua Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.

Wanajeshi watatu wametajwa kuwa vinara wa kupanga njama za kuipindua Serikali ya Burundi wakiwamo maofisa wawili wa ngazi za juu wa polisi.

Msemaji wa Ikulu ya Burundi, Gervais Abayeho alisema jana kwamba washtakiwa wengine wanne ni maofisa wenye vyeo vya chini na wanane ni wanajeshi wa kawaida.

Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya kukamatwa kwa Meja Jenerali Godefroid Niyombare ambaye aliongoza mapinduzi hayo.

Askaribi hao wanatuhumiwa kufanya jaribio la kumpindua Rais Nkurunziza wakipinga  uamuzi wake wa kugombea urais kwa muhula wa tatu.

Abayeho alisema wakati maandamano yakiendelea Bujumbura kupinga uamuzi wa Chama cha CNDD-FDD kumteua Nkurunziza kugombea nafasi hiyo kwa mara nyingine,  Meja Jenerali Niyombare alitangaza kutomtambua Nkurunziza kama rais wa nchi hiyo. Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao walisema kwamba baada ya wateja wao kukamatwa waliteswa na kuumizwa.

 “Wamepigwa na ukiwatazama wamechoka na hawana mashati wala viatu,” alisema mmoja wa mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao kutoka Kampuni ya Mawakili ya Bar, Miburo Anatole.

Anatole alisema anamwakilisha Meja Jenerali Cyrille Ndayirukiye ambaye alikuwa waziri wa zamani wa ulinzi wa nchi hiyo na maofisa wawili wa polisi.

Wakili mwingine, Cyriaque Nibitegeka alisema mteja wake ambaye ni ofisa wa jeshi la nchi hiyo alilazimishwa kwa mtutu wa bunduki kukiri kwamba alihusika kuipindua nchi hiyo. Alisema mteja huyo amegoma kula tangu walipokamatwa wiki iliyopita.

Taarifa zilieleza kwamba endapo watuhumiwa hao watapatikana na hatia watahukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.

Ijumaa iliyopita, Nkurunziza alirejea mjini Bujumbura akitokea Tanzania, huku maandamano ya kumpinga yakiendelea.

Licha ya Serikali kuzuia kufanyika kwa maandamano, waandamanaji vikiwamo vyama vya upinzani na wananchi wameapa kuendelea hadi Rais Nkurunziza atakapotangaza kuacha mpango wake wa kugombea tena urais.
“Tutaendelea kufanya maandamano kwa kuwa malengo yetu ni kumtaka Nkurunziza aache kugombea urais muhula wa tatu. Tunaona wanajaribu kuzuia maandamano yetu, lakini sisi hatutasitisha maandamano. Tutaendelea kuipigania katiba ili iheshimike,” alisema Jean Paul Ndayiragije.
Uchaguzi mkuu nchini humo unatarajiwa kufanyika Juni 26, mwaka huu.
Jaribio la kumpindua Rais Nkurunziza lilitekelezwa na Meja Jenerali Niyombare na maofisa wenzake wa jeshi wakati Nkurunziza akiwa nchini Tanzania kuhudhuria mkutano wa dharura kuhusu mgogoro unaendelea nchini humo, lakini mapinduzi hayo yalizimwa na maofisa wa jeshi wanaomtii.
Idadi ya wakimbizi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani wa Tanzania, Isaac Nantanga alisema Serikali imetoa ushirikiano mzuri katika shughuli ya  kuwapokea wakimbizi wanaotoka Burundi.
Zaidi ya watu 105,000 wameikimbia Burundi, 70,000 wameingia Tanzania na 26, 300 wamekimbilia Rwanda tangu kuanza kwa vurugu nchini humo. Wakimbizi wengi wanaishi katika Kambi ya Mahama.
“Taarifa zinaeleza kwamba watu 10,000 wako mpakani mwa Tanzania na Burundi wakisubri kuingia katika kambi ya wakimbizi mkoani Kigoma,” lilisema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
Nkurunziza hadharani
Kwa mara ya kwanza, Rais Nkurunziza alionekana hadharani jana, huku akiwa amevaa kaunda suti ya bluu. Alionekana akitabasamu, huku akiwasalimia waandishi wa habari na kuzungumza masuala ya ugaidi bila kugusia jaribio la kuipindua serikali yake.
Rais Nkurunziza alizungumzia tishio la ugaidi ambalo limetolewa na kundi la   Al-Qaeda ambalo lina uhusiano na wanamgambo wa Al- Shabaab.
“Tumechukua tahadhari dhidi kundi la Al-Shabaab, tishio hili tumelichukua kwa umakini mkubwa kwa ajili ya usalama wa raia wetu,” alisema Rais Nkurunziza.
Burundi na nchi nyingine za Afrika zimepeleka majeshi ya kulinda amani nchini Somalia.
 Katika tukio jingine, Raia wa Burundi wanaoishi Uingereza wamemuomba Waziri Mkuu wa nchi hiyo, David Cameron kusimamisha misaada ya kifedha kutokana na msimamo wa Rais Nkurunziza.  Raia hao walisema  uamuzi wa Rais Nkurunziza ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.
Watu hao waliandamana juzi jijini London wakipinga Rais Nkurunziza kukiuka katiba na watu 22 waliouawa kwenye maadamano mjini Bujumbura.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba bendera ya nchi hiyo, huku wakitaka Serikali kulinda amani na kumtaka Nkurunziza aache kugombea urais muhula wa tatu.
Kwa mujibu wa Muungano wa Ulaya (EU), Burundi imekuwa ikipewa msaada wa Dola 6 milioni mpaka 9 za Marekani kwa ajili ya kusaidia shughuli za uchaguzi mkuu kila unapowadia.

KIPANYA LEO

WABUNGE CCM SASA NJIAPANDA


 
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Dk  Edward Hoseah akitoa mada kwenye semina ya wabunge iliyofanyika Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herma
Share
Dar/Dodoma. Wakati mkutano wa mwisho wa Bunge la 10 ukiendelea, baadhi ya wabunge CCM wamebaki njiapanda kimaamuzi iwapo waendelee kuikosoa Serikali ya chama chao na kujiweka mahali pazuri kwa wapigakura wao au waifagilie Serikali bila ya kujali hatima ya ubunge wao.
Mkutano huu wa Bajeti utamalizika kwa Bunge kuvunjwa na wabunge kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, hali inayowafanya baadhi yao kuamua kukwepa vikao ‘kuimarisha majimbo yao’ na wengine kulalamika hata kufikisha madai yao kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wakati hali ikiwa hivyo, wenzao wa upinzani wameamua kutumia fursa hiyo kuisulubu Serikali kwa tuhuma na kashfa mbalimbali za nyuma na upungufu wake sasa ikiwamo uandikishaji Daftari la Wapigakura, kuahirishwa Kura ya Maoni, sakata la escrow na dosari zilizotokana katika utekelezaji wa bajeti za maendeleo katika bajeti iliyopita ya mwaka 2014/15.
Hali hiyo inakuja wakati joto la uchaguzi likiwa limepanda huku wapigakura wakiwa na hamu kusikia wawakilishi wao wamevuna kitu gani na jinsi gani wanaiwajibisha Serikali lakini, wawakilishi hao wakitakiwa kuisafisha Serikali ili kukiwekea chama chao mazingira mazuri katika uchaguzi wa Oktoba 25.
Tangu kuanza kwa vikao vya bajeti, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema ni wabunge wachache tu wa CCM ambao wameonekana kuitetea Serikali dhidi ya tuhuma zinazoibuliwa, tofauti na ilivyokuwa katika mikutano iliyopita.
Pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kuwa mstari wa mbele kukemea udhaifu wa watendaji wa Serikali, baadhi ya wabunge wanahofia kukatwa majina yao endapo wataiwajibisha Serikali ya chama chao.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wanaonekana kutoyumba na kuendelea na msimamo wao wa kuikosoa na kuiwajibisha Serikali, wakiwamo Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli ambaye amenukuliwa akilalamika kutishiwa kukatwa jina na viongozi wa chama hicho, Ester Bulaya (Viti maalumu) na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe na Kangi Lugola wa Mwibara.
Mtazamo wa kisomi
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alisema kila chama cha siasa huwa kinaweka ajenda ya uwajibikaji wa pamoja kwa masilahi ya chama hicho.
Dk Makulilo alisema siyo Tanzania pekee, bali hata vyama vingine tawala barani Afrika na Uingereza, vimekuwa na utaratibu wa kukubaliana mambo ya kusimamia kauli ya pamoja.
“Kuna kitu kinaitwa ‘party discipline’ ndani ya chama lakini kuna mambo wanayoweza kuyaacha yajadiliwe kwa uhuru wa kila mbunge na kuna mambo ambayo lazima waonyeshe msimamo wa pamoja,” alisema na kuongeza:
“Sasa wabunge wanaweza kuwa kwenye wakati mgumu kama msimamo wa chama unakinzana na mtazamo wa wapigakura wa mbunge fulani. Hata hivyo, bado kwa siasa ya Tanzania haiwezi kuwa kikwazo cha kukosa ubunge kwani wengi hutumia rushwa zaidi.”

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania(Jukata), Deus Kibamba alisema licha ya ujasiri kwa baadhi ya wabunge wa CCM, wengine wamekuwa na hofu ya kukatwa majina.
“Kitanzi kikubwa kilichopo, huwezi kuwa mbunge mpaka ukubalike ndani ya CCM, lakini mwaka 2010 walikata majina wabunge wengi matokeo yake wananchi wakachagua upinzani, yaani chama kilichagua wagombea ambao ni tofauti na chaguo lao.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Sayansi ya Siasa, Emmanuel Mallya alisema hali ilivyo kwa sasa ni lazima mbunge atazame upepo wa pande zote mbili hususan ndani jimbo lake.
“Hakuna mbunge anayetaka kwa sasa kuonekana akitetea mambo yasiyokubalika kwa wapigakura wake iwapo anahitaji kuomba kura tena, lakini kama hana shida ya kurudi jimboni, basi anaweza kuishambulia Serikali kwa vyovyote au kuisifia kwa namna yoyote,” alisema na kuongeza: “Kuhusu kuadhibiwa na chama chake hiyo haiwezekani kwani hata CCM wanapima hoja na kuangalia upepo wa kukubalika kwa mtu jimboni.”
Hata hivyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba (Viti Maalumu -CCM), alisema haoni mazingira magumu kwa mbunge wa CCM kuitetea Serikali kwani ni maoni yake huru yanayohitaji kuheshimiwa.
“Bunge ni mapambano kati ya upinzani na CCM, lakini suala la kuikosoa Serikali liko palepale kwa wabunge wa CCM na ndiyo maana tunaishauri, kuikumbusha na kisha tunaunga mkono kwa kuamini Serikali ijayo itashughulikia kero za wananchi zilizobakia jimboni,” alisema Simba.
Nape alisema siyo kweli kwamba wabunge wa CCM ndiyo wamekuwa na wakati mgumu, bali wamekuwa huru kuiwajibisha Serikali na ndiyo maana wamekuwa wakiibua tuhuma mbalimbali za ufisadi.
“Kwa hivyo siyo sawa kabisa kusema wabunge wa CCM wana wakati mgumu, mbona hamsemi kuhusu tuhuma za wabunge wa upinzani kwenye majimbo yao?” alisema Nape na kuongeza:
“Asilimia 78 ya wabunge ni wa CCM lakini wanaruhusu na kuibua ufisadi, kama wangekuwa na wakati mgumu wangekuwa wanapitisha? Siyo sawa kabisa kujenga mtazamo huo.”
Wamlilia Dk Hoseah
Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge wa CCM jana walimlilia Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea wakitaka awasaidie kukomesha rafu na rushwa zinavyofanywa na wenyeviti wa chama hicho wa wilaya
na baadhi ya viongozi wa Serikali.

Walitoa kilio hicho kwenye semina ya wabunge iliyoandaliwa na Chama cha Wabunge cha Kupambana na Rushwa (APNAC) mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wabunge baadhi ya mawaziri.
Wakichangia katika semina hiyo wabunge hao walisema rafu na rushwa zimekuwa zikifanyika hadharani majimboni miezi mitatu iliyopita.
Mbunge wa Nkasi Kusini (CCM), Desderius Mipata alisema alitoa taarifa kwa Takukuru kuhusu mmoja ya kiongozi wa Serikali  kujihusisha na kampeni kabla ya muda lakini hajapata mrejesho.
“Huyu anatumia gari, mafuta na dereva wa Serikali kuzunguka vijijini katika jimbo langu. Hivi mimi sina haki ya kujua kinachoendelea maana ninayemtuhumu anapata taarifa kutoka makao makuu juu ya yanayoendelea.”
Mbunge wa pili kulalamika ni wa Igalula, (CCM), Dk Athuman Mfutakamba aliyesema mwenyekiti wa CCM wilayani kwake ambaye ameonyesha nia ya kugombea katika jimbo lake ameanza kugawa sare kwa kisingizio kuwa anatekeleza ahadi zake... “Takukuru mfike na huko muangalie yanayofanyika kwa kisingizio cha kutekeleza ahadi..”
Pia alisema kuna mgombea ambaye alimshinda katika kura za maoni mwaka 2010, ameanzisha vikundi vya kusaidia wanawake na vijana.
“Huyu naye aangaliwe kwa sababu mimi ninaamini kuwa hiyo ni rushwa,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Abia Nyabakari alisema mwenyekiti wa CCM wa wilaya (hakuitaja) alimpigia simu na kumweleza kuwa amemwona akipitapita katika jimbo la Manyovu wilayani Kasulu akiwa na gari lake la kijani.
“Nilimwambia mimi hata sipo huko anakosema lakini aliendelea kunieleza kuwa nifahamu hilo jimbo ni la Obama (Mbunge wa sasa Albert Obama Ntabaliba,” alilalamika.
Alisema Januari 26 mwaka huu kulifanyika kikao cha halmashauri ya wilaya na kiongozi mmoja aliwaambia wajumbe kuwa amepewa fedha na mama mmoja kwa ajili ya kuwanunulia chakula.
Alisema baada ya kula aliwaambia wajumbe wahakikishe mama huyo anapita na kuonya atakayezuia mama hiyo kupita maana ataadhibiwa hata kupoteza uanachama.
“Alisema atakayemzuia mama huyo kupita katika ubunge atahakikisha hafiki popote, ikiwezekana hata kufutiwa uanachama. Mimi ninatishwa na yeye ni kiongozi wa kuidhinisha wagombea,” alisema.

Hata hivyo, malalamiko ya mbunge huyo yalikatishwa na kelele za wabunge waliomtaka kupeleka hoja
hiyo kwenye vikao vya chama kwa kuwa hapo hapakuwa si mahali pake.
“Hayo malalamiko yako uyapeleke katika vikao vya chama chako vikashughulikiwe,” alisema Ezekiah Wenje (Nyamagana - Chadema) na kuungwa mkono na wabunge wengine.
Mbunge wa Nkenge, (CCM), Assumpta Mshama alisema rushwa iko njenje na katika kipindi hiki Bunge linaendelea, kwa kuwa kwenye jimbo lake kuna watu waliitwa na kupatiwa Sh10,000 kila mmoja hadharani.
“Watu wanaahidi kutengeneza vyoo, barabara wanatengeneza… Watu wako (watumishi wa Takukuru) wamekaa muda mrefu wamezoeleka. Kwa nini sasa hivi msiwabadilishe?” alihoji Mshama.
Sheria ya Gharama ya uchaguzi
Wabunge hao pia walilalamikia sheria ya Gharama za Uchaguzi kutoendana na hali halisi.
Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini - Chadema), Felix Mkosamali (Muhambwe - NCCR- Mageuzi) na Wenje, walisema kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi,  bidhaa na huduma zimepanda bei na kuifanya sheria hiyo kutokuwa na uhalisia katika hali ya sasa.
“Watu wataleta risiti kuwa wametumia Sh50 milioni kumbe ukienda katika uhalisia unakuta ametumia Sh200 milioni. Kama haitafanyiwa marekebisho kabla uchaguzi utekelezaji wake hautakuwa na uhalisia,” alisema Wenje.
Rushwa ya Mtandao
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy alisema baadhi ya wagombea wamekuwa wakitumia mitandao kugawa rushwa na kuihoji jinsi Takukuru itakavyowadhibiti.
Mbunge wa Simanjiro(CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema Ikulu imewasafisha waliohusishwa na tuhuma za Akaunti ya Tegeta Escrow na kuhoji iwapo kitendo hicho hakitaathiri Takukuru na uchunguzi wake.

Akijibu hoja hizo, Dk Hoseah alisema taasisi yake haikurupuki katika kuwakamata watuhumiwa wa rushwa na imekuwa ikifanya uchunguzi wa kina kabla ya kuwakamata.
“Wale mnaotumia mitandao ya simu kutuma rushwa mtaumia vibaya katika uchaguzi huu. Ukituma tu rekodi inajionyesha labda sijui utumie lugha gani? Lakini ni rahisi sana kuwapata hawa wa mtandao kuliko wa guest (nyumba za kulala wageni),” alisema.
Kuhusu escrow alisema si kazi ya Takukuru kuwasafisha watuhumiwa, yenyewe inapeleka shauri kwenye mahakama ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuamua.
“Tunaendelea na uchunguzi na kwa wale walioko mahakamani wataendelea kujibu huko. Hatuna mpango wa kufuta kesi sisi tunafuata sheria inavyotuelekeza,” alisema. Kuhusu watendaji wa taasisi yake kukaa sehemu moja miaka mingi alisema kuanzia Januari hadi sasa wametumia Sh1 bilioni kuwahamisha.... “Huwezi kuhamisha mtumishi mmoja tu ni lazima uhamishe watatu na gharama ya kuhamisha mtumishi mmoja si chini ya Sh7 milioni. Hii inatosha sasa maana tukiendelea kuwahamisha tutakosa fedha za kufanya kazi.”
  Chanzo;Mwananchi

SERIKALI YAJIVIKA MWIBA WA BVR


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama

PAMOJA na kazi ya uandikishaji wapiga kura katika daftari la kudumu kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) kuambatana na kasoro lukuki, Serikali imeahidi kuwa kazi hiyo itakamilika ndani ya siku 60. 
Jenista Mhagama-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu wa Bunge), ndiye ametoa ahadi hiyo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba ya Bajeti kwa ofisi ya waziri mkuu 2015/16.
Amesema “ndani ya siku 60 (miezi miwili), kazi hiyo itakuwa imekamilika kutokana na kuongezwa kwa mashine za BVR. Kwa sasa zipo BVR kits 4,850 na serikali inategemea kupokea zingine 3,150 ili kufikisha jumla 8,000.”
Kwa mujibu wa Mhagama, baadhi ya mikoa kama Njombe, uandikishaji tayari umekamilika.
Ameongeza kuwa, kutoka na kuwepo kwa idadi hiyo ya mashine, kuna uwezekano wa kuandikisha watu 800,000 kwa siku iwapo kila mashine moja itaweza kuandikisha watu 100.
“Iwapo mashine hizo zikitumiaka kuandikisha watu 100 kwa siku, hivyo ni wazi kuwa ndani ya siku 60 kazi ya uandikishaji katika daftari la kudumu la mpiga kura litakuwa limekamilika.
Ametaja mikoa mingine ambayo inatarajiwa kuanza kuandikishwa Mei 18 mwaka huu, kuwa ni Dodoma, Singida, Mbeya, Rukwa, Kigoma, Kagera, Katavi na Tabora.
Amesema kuwa kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na uandikishaji katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Kuhusu mshauri juu ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura na kutumia mashine za BVR, Mhagama amesema kuwa, walikataa ushauri huo kutokana na kubaini kuwa ilikuwa ni gharama kubwa zaidi.
Amefafanua kuwa, jinsi mshauri huyo kutoka Marekani alivyowashauri, ilionekana kuwa gharama ingekuwa zadi ya Sh. 321 bilioni badala ya Sh. 293 za sasa.
“Ikumbukwe kuwa uboreshaji daftari mwaka jana, uligharimu Sh. 72 bilioni na kama matumizi ya mashine ni Sh. 218 bilioni, jumla zingekuwa Sh. 321 bilioni,”amesema.
Akizungumzia uchaguzi wa Zanzibar, Mhagama amesema “masuala ya uchaguzi yatasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Hata hivyo, uhakika ni kwamba daftari litaboreshwa zaidi.”  
Kwa mujibu wa Mhagama, wapinzani wamekuwa wakilalamikia juu uboreshwaji wa daftari ya kudumu la wapiga kura na kuhofia uchaguzi mkuu ujao kutofanyika.
 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger