Home » » 17 MAHAKAMANI KWA JARIOBIO LA KUMPINDUA NKURUNZIZA

17 MAHAKAMANI KWA JARIOBIO LA KUMPINDUA NKURUNZIZA



 

 
Bujumbura, Burundi. Maofisa 17 wa Jeshi la Burundi wametiwa mbaroni wakiwamo majenerali watano na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuipindua Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.

Wanajeshi watatu wametajwa kuwa vinara wa kupanga njama za kuipindua Serikali ya Burundi wakiwamo maofisa wawili wa ngazi za juu wa polisi.

Msemaji wa Ikulu ya Burundi, Gervais Abayeho alisema jana kwamba washtakiwa wengine wanne ni maofisa wenye vyeo vya chini na wanane ni wanajeshi wa kawaida.

Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya kukamatwa kwa Meja Jenerali Godefroid Niyombare ambaye aliongoza mapinduzi hayo.

Askaribi hao wanatuhumiwa kufanya jaribio la kumpindua Rais Nkurunziza wakipinga  uamuzi wake wa kugombea urais kwa muhula wa tatu.

Abayeho alisema wakati maandamano yakiendelea Bujumbura kupinga uamuzi wa Chama cha CNDD-FDD kumteua Nkurunziza kugombea nafasi hiyo kwa mara nyingine,  Meja Jenerali Niyombare alitangaza kutomtambua Nkurunziza kama rais wa nchi hiyo. Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao walisema kwamba baada ya wateja wao kukamatwa waliteswa na kuumizwa.

 “Wamepigwa na ukiwatazama wamechoka na hawana mashati wala viatu,” alisema mmoja wa mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao kutoka Kampuni ya Mawakili ya Bar, Miburo Anatole.

Anatole alisema anamwakilisha Meja Jenerali Cyrille Ndayirukiye ambaye alikuwa waziri wa zamani wa ulinzi wa nchi hiyo na maofisa wawili wa polisi.

Wakili mwingine, Cyriaque Nibitegeka alisema mteja wake ambaye ni ofisa wa jeshi la nchi hiyo alilazimishwa kwa mtutu wa bunduki kukiri kwamba alihusika kuipindua nchi hiyo. Alisema mteja huyo amegoma kula tangu walipokamatwa wiki iliyopita.

Taarifa zilieleza kwamba endapo watuhumiwa hao watapatikana na hatia watahukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.

Ijumaa iliyopita, Nkurunziza alirejea mjini Bujumbura akitokea Tanzania, huku maandamano ya kumpinga yakiendelea.

Licha ya Serikali kuzuia kufanyika kwa maandamano, waandamanaji vikiwamo vyama vya upinzani na wananchi wameapa kuendelea hadi Rais Nkurunziza atakapotangaza kuacha mpango wake wa kugombea tena urais.
“Tutaendelea kufanya maandamano kwa kuwa malengo yetu ni kumtaka Nkurunziza aache kugombea urais muhula wa tatu. Tunaona wanajaribu kuzuia maandamano yetu, lakini sisi hatutasitisha maandamano. Tutaendelea kuipigania katiba ili iheshimike,” alisema Jean Paul Ndayiragije.
Uchaguzi mkuu nchini humo unatarajiwa kufanyika Juni 26, mwaka huu.
Jaribio la kumpindua Rais Nkurunziza lilitekelezwa na Meja Jenerali Niyombare na maofisa wenzake wa jeshi wakati Nkurunziza akiwa nchini Tanzania kuhudhuria mkutano wa dharura kuhusu mgogoro unaendelea nchini humo, lakini mapinduzi hayo yalizimwa na maofisa wa jeshi wanaomtii.
Idadi ya wakimbizi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani wa Tanzania, Isaac Nantanga alisema Serikali imetoa ushirikiano mzuri katika shughuli ya  kuwapokea wakimbizi wanaotoka Burundi.
Zaidi ya watu 105,000 wameikimbia Burundi, 70,000 wameingia Tanzania na 26, 300 wamekimbilia Rwanda tangu kuanza kwa vurugu nchini humo. Wakimbizi wengi wanaishi katika Kambi ya Mahama.
“Taarifa zinaeleza kwamba watu 10,000 wako mpakani mwa Tanzania na Burundi wakisubri kuingia katika kambi ya wakimbizi mkoani Kigoma,” lilisema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
Nkurunziza hadharani
Kwa mara ya kwanza, Rais Nkurunziza alionekana hadharani jana, huku akiwa amevaa kaunda suti ya bluu. Alionekana akitabasamu, huku akiwasalimia waandishi wa habari na kuzungumza masuala ya ugaidi bila kugusia jaribio la kuipindua serikali yake.
Rais Nkurunziza alizungumzia tishio la ugaidi ambalo limetolewa na kundi la   Al-Qaeda ambalo lina uhusiano na wanamgambo wa Al- Shabaab.
“Tumechukua tahadhari dhidi kundi la Al-Shabaab, tishio hili tumelichukua kwa umakini mkubwa kwa ajili ya usalama wa raia wetu,” alisema Rais Nkurunziza.
Burundi na nchi nyingine za Afrika zimepeleka majeshi ya kulinda amani nchini Somalia.
 Katika tukio jingine, Raia wa Burundi wanaoishi Uingereza wamemuomba Waziri Mkuu wa nchi hiyo, David Cameron kusimamisha misaada ya kifedha kutokana na msimamo wa Rais Nkurunziza.  Raia hao walisema  uamuzi wa Rais Nkurunziza ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.
Watu hao waliandamana juzi jijini London wakipinga Rais Nkurunziza kukiuka katiba na watu 22 waliouawa kwenye maadamano mjini Bujumbura.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba bendera ya nchi hiyo, huku wakitaka Serikali kulinda amani na kumtaka Nkurunziza aache kugombea urais muhula wa tatu.
Kwa mujibu wa Muungano wa Ulaya (EU), Burundi imekuwa ikipewa msaada wa Dola 6 milioni mpaka 9 za Marekani kwa ajili ya kusaidia shughuli za uchaguzi mkuu kila unapowadia.
Toa maoni yako kwa habari hii kwa kuweka email yako hapa,na endelea kutufatilia zaidi Ukurasa wa habari

0 comments:

 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger