Dar/Dodoma. Wakati mkutano wa
mwisho wa Bunge la 10 ukiendelea, baadhi ya wabunge CCM wamebaki
njiapanda kimaamuzi iwapo waendelee kuikosoa Serikali ya chama chao na
kujiweka mahali pazuri kwa wapigakura wao au waifagilie Serikali bila ya
kujali hatima ya ubunge wao.
Mkutano huu wa Bajeti utamalizika kwa Bunge
kuvunjwa na wabunge kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, hali inayowafanya
baadhi yao kuamua kukwepa vikao ‘kuimarisha majimbo yao’ na wengine
kulalamika hata kufikisha madai yao kwenye Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wakati hali ikiwa hivyo, wenzao wa upinzani
wameamua kutumia fursa hiyo kuisulubu Serikali kwa tuhuma na kashfa
mbalimbali za nyuma na upungufu wake sasa ikiwamo uandikishaji Daftari
la Wapigakura, kuahirishwa Kura ya Maoni, sakata la escrow na dosari
zilizotokana katika utekelezaji wa bajeti za maendeleo katika bajeti
iliyopita ya mwaka 2014/15.
Hali hiyo inakuja wakati joto la uchaguzi likiwa
limepanda huku wapigakura wakiwa na hamu kusikia wawakilishi wao
wamevuna kitu gani na jinsi gani wanaiwajibisha Serikali lakini,
wawakilishi hao wakitakiwa kuisafisha Serikali ili kukiwekea chama chao
mazingira mazuri katika uchaguzi wa Oktoba 25.
Tangu kuanza kwa vikao vya bajeti, wachambuzi wa
masuala ya kisiasa wanasema ni wabunge wachache tu wa CCM ambao
wameonekana kuitetea Serikali dhidi ya tuhuma zinazoibuliwa, tofauti na
ilivyokuwa katika mikutano iliyopita.
Pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kuwa mstari wa mbele
kukemea udhaifu wa watendaji wa Serikali, baadhi ya wabunge wanahofia
kukatwa majina yao endapo wataiwajibisha Serikali ya chama chao.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wanaonekana
kutoyumba na kuendelea na msimamo wao wa kuikosoa na kuiwajibisha
Serikali, wakiwamo Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli ambaye
amenukuliwa akilalamika kutishiwa kukatwa jina na viongozi wa chama
hicho, Ester Bulaya (Viti maalumu) na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe
na Kangi Lugola wa Mwibara.
Mtazamo wa kisomi
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alisema kila chama
cha siasa huwa kinaweka ajenda ya uwajibikaji wa pamoja kwa masilahi ya
chama hicho.
Dk Makulilo alisema siyo Tanzania pekee, bali hata
vyama vingine tawala barani Afrika na Uingereza, vimekuwa na utaratibu
wa kukubaliana mambo ya kusimamia kauli ya pamoja.
“Kuna kitu kinaitwa ‘party discipline’ ndani ya
chama lakini kuna mambo wanayoweza kuyaacha yajadiliwe kwa uhuru wa kila
mbunge na kuna mambo ambayo lazima waonyeshe msimamo wa pamoja,”
alisema na kuongeza:
“Sasa wabunge wanaweza kuwa kwenye wakati mgumu
kama msimamo wa chama unakinzana na mtazamo wa wapigakura wa mbunge
fulani. Hata hivyo, bado kwa siasa ya Tanzania haiwezi kuwa kikwazo cha
kukosa ubunge kwani wengi hutumia rushwa zaidi.”
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania(Jukata), Deus Kibamba
alisema licha ya ujasiri kwa baadhi ya wabunge wa CCM, wengine wamekuwa
na hofu ya kukatwa majina.
“Kitanzi kikubwa kilichopo, huwezi kuwa mbunge
mpaka ukubalike ndani ya CCM, lakini mwaka 2010 walikata majina wabunge
wengi matokeo yake wananchi wakachagua upinzani, yaani chama kilichagua
wagombea ambao ni tofauti na chaguo lao.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (OUT), ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Sayansi ya Siasa, Emmanuel
Mallya alisema hali ilivyo kwa sasa ni lazima mbunge atazame upepo wa
pande zote mbili hususan ndani jimbo lake.
“Hakuna mbunge anayetaka kwa sasa kuonekana
akitetea mambo yasiyokubalika kwa wapigakura wake iwapo anahitaji kuomba
kura tena, lakini kama hana shida ya kurudi jimboni, basi anaweza
kuishambulia Serikali kwa vyovyote au kuisifia kwa namna yoyote,”
alisema na kuongeza: “Kuhusu kuadhibiwa na chama chake hiyo haiwezekani
kwani hata CCM wanapima hoja na kuangalia upepo wa kukubalika kwa mtu
jimboni.”
Hata hivyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto, Sophia Simba (Viti Maalumu -CCM), alisema haoni mazingira
magumu kwa mbunge wa CCM kuitetea Serikali kwani ni maoni yake huru
yanayohitaji kuheshimiwa.
“Bunge ni mapambano kati ya upinzani na CCM,
lakini suala la kuikosoa Serikali liko palepale kwa wabunge wa CCM na
ndiyo maana tunaishauri, kuikumbusha na kisha tunaunga mkono kwa kuamini
Serikali ijayo itashughulikia kero za wananchi zilizobakia jimboni,”
alisema Simba.
Nape alisema siyo kweli kwamba wabunge wa CCM
ndiyo wamekuwa na wakati mgumu, bali wamekuwa huru kuiwajibisha Serikali
na ndiyo maana wamekuwa wakiibua tuhuma mbalimbali za ufisadi.
“Kwa hivyo siyo sawa kabisa kusema wabunge wa CCM
wana wakati mgumu, mbona hamsemi kuhusu tuhuma za wabunge wa upinzani
kwenye majimbo yao?” alisema Nape na kuongeza:
“Asilimia 78 ya wabunge ni wa CCM lakini
wanaruhusu na kuibua ufisadi, kama wangekuwa na wakati mgumu wangekuwa
wanapitisha? Siyo sawa kabisa kujenga mtazamo huo.”
Wamlilia Dk Hoseah
Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge wa CCM
jana walimlilia Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea wakitaka
awasaidie kukomesha rafu na rushwa zinavyofanywa na wenyeviti wa chama
hicho wa wilaya
na baadhi ya viongozi wa Serikali.
Walitoa kilio hicho kwenye semina ya wabunge iliyoandaliwa na
Chama cha Wabunge cha Kupambana na Rushwa (APNAC) mjini Dodoma na
kuhudhuriwa na wabunge baadhi ya mawaziri.
Wakichangia katika semina hiyo wabunge hao
walisema rafu na rushwa zimekuwa zikifanyika hadharani majimboni miezi
mitatu iliyopita.
Mbunge wa Nkasi Kusini (CCM), Desderius Mipata
alisema alitoa taarifa kwa Takukuru kuhusu mmoja ya kiongozi wa
Serikali kujihusisha na kampeni kabla ya muda lakini hajapata mrejesho.
“Huyu anatumia gari, mafuta na dereva wa Serikali
kuzunguka vijijini katika jimbo langu. Hivi mimi sina haki ya kujua
kinachoendelea maana ninayemtuhumu anapata taarifa kutoka makao makuu
juu ya yanayoendelea.”
Mbunge wa pili kulalamika ni wa Igalula, (CCM), Dk
Athuman Mfutakamba aliyesema mwenyekiti wa CCM wilayani kwake ambaye
ameonyesha nia ya kugombea katika jimbo lake ameanza kugawa sare kwa
kisingizio kuwa anatekeleza ahadi zake... “Takukuru mfike na huko
muangalie yanayofanyika kwa kisingizio cha kutekeleza ahadi..”
Pia alisema kuna mgombea ambaye alimshinda katika kura za maoni mwaka 2010, ameanzisha vikundi vya kusaidia wanawake na vijana.
“Huyu naye aangaliwe kwa sababu mimi ninaamini kuwa hiyo ni rushwa,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Abia Nyabakari
alisema mwenyekiti wa CCM wa wilaya (hakuitaja) alimpigia simu na
kumweleza kuwa amemwona akipitapita katika jimbo la Manyovu wilayani
Kasulu akiwa na gari lake la kijani.
“Nilimwambia mimi hata sipo huko anakosema lakini
aliendelea kunieleza kuwa nifahamu hilo jimbo ni la Obama (Mbunge wa
sasa Albert Obama Ntabaliba,” alilalamika.
Alisema Januari 26 mwaka huu kulifanyika kikao cha
halmashauri ya wilaya na kiongozi mmoja aliwaambia wajumbe kuwa amepewa
fedha na mama mmoja kwa ajili ya kuwanunulia chakula.
Alisema baada ya kula aliwaambia wajumbe
wahakikishe mama huyo anapita na kuonya atakayezuia mama hiyo kupita
maana ataadhibiwa hata kupoteza uanachama.
“Alisema atakayemzuia mama huyo kupita katika
ubunge atahakikisha hafiki popote, ikiwezekana hata kufutiwa uanachama.
Mimi ninatishwa na yeye ni kiongozi wa kuidhinisha wagombea,” alisema.
Hata hivyo, malalamiko ya mbunge huyo yalikatishwa na kelele za wabunge waliomtaka kupeleka hoja
hiyo kwenye vikao vya chama kwa kuwa hapo hapakuwa si mahali pake.
“Hayo malalamiko yako uyapeleke katika vikao vya
chama chako vikashughulikiwe,” alisema Ezekiah Wenje (Nyamagana -
Chadema) na kuungwa mkono na wabunge wengine.
Mbunge wa Nkenge, (CCM), Assumpta Mshama alisema
rushwa iko njenje na katika kipindi hiki Bunge linaendelea, kwa kuwa
kwenye jimbo lake kuna watu waliitwa na kupatiwa Sh10,000 kila mmoja
hadharani.
“Watu wanaahidi kutengeneza vyoo, barabara
wanatengeneza… Watu wako (watumishi wa Takukuru) wamekaa muda mrefu
wamezoeleka. Kwa nini sasa hivi msiwabadilishe?” alihoji Mshama.
Sheria ya Gharama ya uchaguzi
Wabunge hao pia walilalamikia sheria ya Gharama za Uchaguzi kutoendana na hali halisi.
Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini - Chadema),
Felix Mkosamali (Muhambwe - NCCR- Mageuzi) na Wenje, walisema kutokana
na kushuka kwa thamani ya shilingi, bidhaa na huduma zimepanda bei na
kuifanya sheria hiyo kutokuwa na uhalisia katika hali ya sasa.
“Watu wataleta risiti kuwa wametumia Sh50 milioni
kumbe ukienda katika uhalisia unakuta ametumia Sh200 milioni. Kama
haitafanyiwa marekebisho kabla uchaguzi utekelezaji wake hautakuwa na
uhalisia,” alisema Wenje.
Rushwa ya Mtandao
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy
alisema baadhi ya wagombea wamekuwa wakitumia mitandao kugawa rushwa na
kuihoji jinsi Takukuru itakavyowadhibiti.
Mbunge wa Simanjiro(CCM), Christopher Ole Sendeka,
alisema Ikulu imewasafisha waliohusishwa na tuhuma za Akaunti ya Tegeta
Escrow na kuhoji iwapo kitendo hicho hakitaathiri Takukuru na uchunguzi
wake.
Akijibu hoja hizo, Dk Hoseah alisema taasisi yake haikurupuki
katika kuwakamata watuhumiwa wa rushwa na imekuwa ikifanya uchunguzi wa
kina kabla ya kuwakamata.
“Wale mnaotumia mitandao ya simu kutuma rushwa
mtaumia vibaya katika uchaguzi huu. Ukituma tu rekodi inajionyesha labda
sijui utumie lugha gani? Lakini ni rahisi sana kuwapata hawa wa mtandao
kuliko wa guest (nyumba za kulala wageni),” alisema.
Kuhusu escrow alisema si kazi ya Takukuru
kuwasafisha watuhumiwa, yenyewe inapeleka shauri kwenye mahakama ambayo
ndiyo yenye mamlaka ya kuamua.
“Tunaendelea na uchunguzi na kwa wale walioko
mahakamani wataendelea kujibu huko. Hatuna mpango wa kufuta kesi sisi
tunafuata sheria inavyotuelekeza,” alisema. Kuhusu watendaji wa taasisi
yake kukaa sehemu moja miaka mingi alisema kuanzia Januari hadi sasa
wametumia Sh1 bilioni kuwahamisha.... “Huwezi kuhamisha mtumishi mmoja
tu ni lazima uhamishe watatu na gharama ya kuhamisha mtumishi mmoja si
chini ya Sh7 milioni. Hii inatosha sasa maana tukiendelea kuwahamisha
tutakosa fedha za kufanya kazi.”
0 comments:
Post a Comment