GOLIKIPA wa kimataifa wa Tanzania, Deogratius Munishi ‘Dida’ amejiunga na timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Pretoria, inayofahamika kama Tuks FC ya Afrika Kusini.
Timu hiyo yenye maskani yake Hatfield mjini Pretoria kwa sasa inacheza Ligi Daraja la Kwanza nchini Afrika Kusini na inajaribun kuchukua wachezaji wakubwa wenye uzoefu katika jitihada za kurudi Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini.
Dida anajiunga na timu hiyo baada ya kumaliza mkataba wake Yanga SC na kuamua mwenyewe kuondoka ili kwenda kusaka changamoto mpya baada ya kucheza Tanzania kwa muda mrefu.
Dida amedakia klabu zote kubwa Tanzania, kuanzia Simba, Azam FC, Mtibwa Sugar na Yanga baada ya kuibukia Manyema FC, wakati pia amewahi kucheza soka ya kulipwa Oman.
Deogratius Munishi ‘Dida’ amejiunga na Tuks FC ya Ligi Daraja la Kwanza Afrika Kusini
Katika timu zote alizowahi kudakia, Dida alikuwa kipa namba moja, kasoro Simba SC pekee ambako alishindwa kumuondoka Juma Kaseja langoni.
Na ni kutokana na kiu yake ya kutaka kudaka, Dida aliamua kuondoka Simba na kwenda Mtibwa Sugar ili apate nafasi ya kucheza.
Dida aliyezaliwa mwaka 1989 Moshi, Kilimanjaro katika familia ya Mzee Bonaventure Munishi (marehemu) na mama Hilda Temu akiwa ni mtoto wa pili katika familia hiyo ya watoto wanne na ndugu zake ni Ismail, Kasija na George.
Alisoma Madenge shule ya msingi kuanzia mwaka 1996 mpaka 2002 kisha kujiunga na Makongo sekondari mwaka uliofuata lakini alisoma kwa mwezi mmoja tu na kujikita katika soka.
Dida akiwa na mshambuliaji wa zamani wa Ivory Coast, Didier Drogba baada ya mechi na Tanzania mwaka 2010 |
Mwaka 2004 alisajiliwa na Coastal Union ya Tanga na kucheza Ligi daraja la kwanza, mwaka uliofuata alijiunga na timu ya Chuoni ya Zanzibar iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza visiwani humo.
Mwaka uliofuata alijiengua katika timu hiyo na kurudi Dar es Salaam na kuendelea kujifua katika viwanja vya Tungi, Temeke. Februari 2007 alijiunga na timu ya Makondeko ya Temeke na kushsiriki Ligi ya Taifa, lakini Machi mwaka huo huo alijiunga na Mkunguni ya Ilala kushiriki Ligi ya Taifa pia.
Hapo hakuka sana kwani Aprili, 2007 alijiunga na Manyema kucheza Ligi Daraja la kwanza na kufanikiwa kuipandisha timu hiyo Ligi Kuu, ndipo Simba ilipomuona na kumsajili mwezi Novemba mwaka huo huo kutokana na uwezo aliouonyesha katika timu hiyo.
Baada ya miaka miwili akaondoka Simba kwenda Mtibwa, baadaye Oman kabla ya kusajiliwa Azam FC ambako alidaka mwaka 2013 alipojiunga na Yanga. Amekuwa kipa wa timu ya taifa tangu mwaka 2009 chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo kabla ya hivi karibuni kuachwa na kocha mzalendo, Salum Mayanga.
0 comments:
Post a Comment