Home » » UKAWA YAKATAA MIZENGWE YA NEC

UKAWA YAKATAA MIZENGWE YA NEC


Viongozi wa Vyama vinavyounda Umoja wa wadai Katiba ya wananchi (UKAWA), Freeman Mbowe (kushoto), James Mbatia (katikati), Prof. Ibrahim Lipumba (wa pili kulia) na Dk. Emmanuel Makaidi
Viongozi wa Vyama vinavyounda Umoja wa wadai Katiba ya wananchi (UKAWA), Freeman Mbowe (kushoto), James Mbatia (katikati), Prof. Ibrahim Lipumba (wa pili kulia) na Dk. Emmanuel Makaidi

VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) leo vimetoa msimamo juu ya njama za kuahirisha uchaguzi mkuu unaotakiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.  

Msimamo huo wameutoa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
UKAWA imesisitiza kwamba kuahirisha Uchaguzi Mkuu ni sawa na kumuongezea  Rais Jakaya Kikwete na Chama cha Mapinduzi (CCM) muda wa kuendelea kutawala.
UKAWA imesema jaribio lolote la kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa kisingizio chochote kile litakuwa kinyume na Katiba ya sasa ya Tanzania na litahesabika sawa na Mapinduzi dhidi ya Katiba.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema ” Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijaanza maandalizi yoyote kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu licha ya kwamba imebaki miezi sita tu Uchaguzi Mkuu ufanyike kwa mujibu wa Katiba”.
Lipumba amesema shughuli zinazohusiana na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu na vifaa vinavyotumika Kwa ajili yake ambavyo kwa taratibu za  miaka yote huanza kufanyika angalau mwaka mmoja na nusu kabla ya siku ya uchaguzi hazijaanza kufanyika, vifaa vinavyoohitaji havijanunuliwa na fedha kwa ajili hiyo hazijategwa hadi sasa.
Aidha, Lipumba amesema “Licha ya madai ya muda mrefu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 imevurugwa kwa makusudi kwa kutokutenga Fedha kwa ajili hiyo katika bajeti ya serikali tangu mwaka 2012″.
“Serikali ya CCM haijatoa fedha kwa NEC kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu. Badala yake NEC imeendelea kutangaza kwamba inafanya maandalizi kwa ajili ya Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa ambayo imepitwa muda kisheria, “amesema Lipumba.
Hivyo Kwa Sheria ya Kura ya Maoni ilivyo kwa sasa, hakuna uwezekano wa Kura ya Maoni kufanyika tena bila kwanza kufanya marekebisho ya sheria hiyo.
Hadi sasa Serikali haijapeleka bungeni Muswada wa Sheria kurekebisha Sheria hiyo ili kuwezesha Kura ya Maoni.
Aidha, Mwenyekiti wa chama cha NCCR  – Mageuzi, James Mbatia amesema “kuruhusu Uchaguzi Mkuu uahirishwe kwa kisingizio chochote ni kuwazawadia wazembe na kuwaongezea mafisadi wanaolimaliza taifa kwa ufisadi muda wa kuendelea na ufisadi”.
” Watu hawa wanafahamu kuwa tumekuwa tukifanya Uchaguzi Mkuu kila baada ya miaka mitano tangu mwaka 1960. Hata mwaka 1980, miezi michache baada ya kutoka vitani dhidi ya Nduli Iddi Amin wa Uganda na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kutangaza miezi 18 ya kujifunga mikanda kwa sababu ya hali mbaya ya uchumi iliyosababishwa na vita ya Uganda, hatukuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo, “amesema Mbatia.
Mwenyekiti wa chama cha National League for Democracy (NLD), Dk. Emmanuel Makaidi amesema “kubadilisha Katiba ya salsa kwa lengo la kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba sio tu kutaathiri misingi muhimu ya Katiba ya sasa, bali pia kutahatarisha amani ya nchi”.
“Tumeona kinachoendelea Burundi baada ya Raid Pierre Nkurunzinza na chama chake kuamua kuamua kujiongezea muda wa kutawala nchi hiyo. Tumeona yanayoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Congo (DRC) baada ya Joseph Kabila kutaka kufanya hivyo. Kikwete na wanaCCM wenzake wasitake kuingiza nchi yetu katika majanga yasiyokuwa na sababu,” ameongeza Makaidi.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema “Tume iliwaahidi watanzania kwamba watu wote wenye sifa wataandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura”.
“Leo Tume inapunguza muda wa siku 14 hadi siku 7 wakati tunafahamu kwamba Tume inavifaa pungufu vya kuandikisha wapiga kura. Hii ni njama ya Tume na serikali kuhakikisha wapiga kura wengi hawaandikishwi,” amesema Mbowe.
Kuhusu mgawanyo ndani ya majimbo. UKAWA imesema kati ya majimbo 239 nchi nzima, tayari wamekubaliana majimbo 227 huku majimbo 12 bado yakiwekewa vigezo kwa ajili ya kugawana.
UKAWA imekana taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu “chama cha NCCR – Mageuzi kimejitoa au kimeandika barua ya kuomba kujitoa kwenye UKAWA.
Toa maoni yako kwa habari hii kwa kuweka email yako hapa,na endelea kutufatilia zaidi Ukurasa wa habari

0 comments:

 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger