KAMATI
Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeazimia na
kulaani tabia ya Rais Jakaya Kikwete kusafiri ovyo nje ya nchi wakati
taifa lipo katika kipindi kigumu na matatizo makubwa ambayo yanahitaji
uongozi thabiti.
Kamati
Kuu ilikutana kwa siku mbili kati ya tarehe 3 hadi 5 Mei mwaka huu, na
kuitaka pia serikali kuchukua hatua za dharura kunusuru shilingi kwani
athari zake ni kubwa sana kiuchumi na kijamii na kwamba zitasababisha
mfumuko wa bei.
Akisoma
maazimio hayo leo kwa waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Chadema
yaliyopo mtaa wa Ufipa Kinondoni, Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa,
amesema kamati kuu vile vile ilipokea na kujadili hali halisi ya sekta
ya usafirishaji nchini.
Amesema
kuwa, wamebaini udhaifu mkubwa ambao upo ndani ya sekta hiyo kutokana
na usimamizi dhaifu wa watu ambao walipewa dhamana kuanzia Waziri wa
Uchukuzi, Samuel Sitta ambaye ameshindwa kabisa.
“Hali
hiyo inasababisha sekta hiyo kukosa mwelekeo na hivyo kuleta madhara
mengi kwa wananchi kutokana na ajali za kila siku kuanzia vyombo vya
majini na barabarani. Kamati kuu imebaini kutokana na mgomo wa madereva
wananchi wameathirika kisaikolojia na kiuchumi,”amesema.
Kwa
mujibu wa Dk. Slaa, Kamati kuu, imeazimia kuunga mkono madai ya
madereva kwani ni halali na hivyo ni lazima serikali iyatekeleze madai
yao yote ya muda mrefu. Amesema “kuendelea kuyapuuza ni kukubali
kuendelea kuhatarisha maisha ya abiria.”
Kuhusu
uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, Dk. Slaa amesema kamati kuu imepokea
taarifa ya kina namna ambavyo hadi sasa maandalizi ya msingi kisheria
hayajafanyika. Ametaja kuwa ni mandalizi ya vifaa, fedha, kutangaza
majimbo na kata mpya, kutangaza vituo na kusuasua kwa uandikishaji
wapiga kura.
“Katika
jambo hili, kamati kuu imeazimia kuwa uchaguzi huo lazima ufanyike
Oktoba kwa mujibu wa Katiba na serikali ya CCM isijiandae kutumia
kisingizio chochote kuahirisha kwa sababu uchaguzi sio jambo la dharura,
bali lilijulikana miaka mitano iliyopita,” amefafanua.
CHANZO MWANAHALISI ONLINE
0 comments:
Post a Comment