Viongozi
wa Chadema wakiomba dua kabla ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu ya
chama hicho kilichofanyika Dar es Salaam jana. Kuanzia kulia ni Makamu
Mwenyekiti, Profesa Abdallah Safari, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe, Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar),
Salum Mwalimu. Picha na Venance Nestory
Dar es
Salaam. Kamati Kuu ya Chadema imepanga Agosti 4 kuwa siku ya kumpata
mgombea wake wa urais ambaye ataingia kwenye kinyang'anyiro cha
kumtafuta mgombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa).
Vyama
vinne vilivyounda Ukawa, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD,
vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa kuanzia ngazi ya urais,
lakini kila chama kitateua mgombea wake kabla ya kukubaliana mtu
atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Ratiba
iliyotolewa jana na Chadema inaonyesha kuwa chama hicho kitatumia siku
76, kuanzia Mei 18, kumaliza mchakato wa kuwapata wagombea wake wa
nafasi za udiwani, ubunge na urais kwa kuhitimisha na Mkutano Mkuu. Kwa
mujibu wa ratiba hiyo, Chadema itampata mgombea wake wa urais takriban
siku 14 zaidi kulinganisha na mwaka 2010 wakati Dk Willibrod Slaa
alipoteuliwa.
Kwa
mujibu wa Ibara ya 7.710 (C) ya katiba ya Chadema, Mkutano Mkuu ndiyo
chombo chenye mamlaka ya kumpitisha mgombea wa urais kwa tiketi ya chama
hicho.
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia wanahabari jana kuwa kamati hiyo
imeridhia mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu uanze ili watia nia
katika maeneo mbalimbali waanze kuchukua fomu za udiwani, uwakilishi na
ubunge.
Katika
ratiba hiyo , chama hicho kimeyapa kipaumbele maeneo yanayoonekana
kutokuwa na madiwani na wabunge, kuanza kuchukua fomu siku ya kwanza ya
kazi hiyo na kuzirudisha Juni 25.
Aidha
ratiba hiyo inaonyesha kuwa makada waliopo kwenye maeneo yenye madiwani
watachukua na kurejesha fomu ndani ya siku 10 kuanzia Julai Mosi.
Wakati
huo, maeneo yenye wabunge kwa sasa yakipatiwa siku tano za kukamilisha
uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo kuanzia Julai 6 hadi 10 huku vigogo
wanaounyemelea urais wakipigiwa kipenga Julai 20 hadi 25.
Mara
baada ya wagombea urais kukamilisha taratibu za kinyang'anyiro, Chadema
imepanga kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea ubunge Agosti 1 na 2 huku
Baraza Kuu likipangwa kukutana siku inayofuata kabla ya Mkutano Mkuu
kukutana Agosti, 4.
Chadema
imeungana na CUF kutangaza ratiba ya kuwapata wanachama watakaowania
uongozi katika Uchaguzi Mkuu ambao kikatiba unatakiwa ufanyike wiki ya
mwisho ya Oktoba na kubakiza mchakato wa kumpata mgombea mmoja kila
nafasi ya uongozi.
Akielezea
zaidi yaliyojiri katika vikao vya kawaida vilivyofanyika Mei 3 na 4
mwaka huu, Mbowe alisema Kamati Kuu ilipokea na kujadili makubaliano
yaliyofikiwa ndani ya Ukawa.
Mbowe,
ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema kuwa kamati hiyo iliwapongeza
viongozi hao kwa hatua walizofikia na kuwataka wamalize masuala machache
yaliyosalia ili wawajulishe Watanzania wanaounga mkono umoja huo wajue
kinachoendelea.CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment