Home » » MREMA APEWA SIKU 80 KUFANYA UCHAGUZI TLP

MREMA APEWA SIKU 80 KUFANYA UCHAGUZI TLP

 


        
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imetoa siku 80 kwa uongozi wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) kuhakikisha kinafanya uchaguzi wake wa ndani wa kuwapata viongozi wapya.

Kauli hiyo imeitolewa baada ya baadhi ya wanachama wa chama hicho kufikisha malalamiko katika ofisi hiyo wakiiomba itangaze kwamba uongozi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema umefikia kikomo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukweli na Maridhiano wa TLP Taifa, Joram Kinanda alimtuhumu Mrema kukiuka katiba ya chama hicho, kuongoza chama kidikteta, kuporomosha heshima ya chama na kujilimbikizia madaraka.

Akizungumza ofisini kwake, Dar es Salaam jana, Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema baada ya kusikiliza pande zote zinazosigana ofisi hiyo iliwataka viongozi kuandaa uchaguzi.
"Tuliwasikiliza wote upande wa Kinanda na upande wa Mrema ambaye alikuwa na sababu kwamba alishindwa kuitisha uchaguzi kutokana na hali yake ya afya lakini tumewaandikia barua kuwa ifikapo Aprili 26 wawe wamekwisha kufanya uchaguzi na si vinginevyo," alisema Nyahoza na kuongeza: "Vyama hivi ili viweze kujinasua na migogoro ya mara kwa mara lazima vijiendeshe kama taasisi na si chama cha mtu mmoja. Hii itasaidia kukuza demokrasia nchini na siku zote demokrasia inaanzia katika vyama vyetu ndipo inakuja juu. kama vyama havina demokrasia ni ngumu hata huku juu kuwapo."

Malalamiko ya Kinanda yalitolewa pia na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Jeremiah Shelukindo aliposema jana kuwa aliamua kuandika barua ya kujiuzulu tangu Desemba 15 mwaka jana kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Mrema. Akizungumzia uamuzi huo Mrema alisema: "Kwanza tunaishukuru Ofisi ya Msajili kwani ilielewa sababu tulizozitoa za kutofanya uchaguzi, katiba yetu inaturuhusu kufanya hivyo na tutatekeleza agizo hilo.

"Ofisi ya Msajili ilituhakikishia lazima tufanye uchaguzi kamati kuu yetu imekubaliana kwamba uchaguzi utafanyika Aprili 26 na maandalizi ya uchaguzi huo yanakwenda vizuri."
Mrema ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo akizungumzia tuhuma za Shelukindo alisema, "Hazina ukweli wowote na tunaendesha chama kwa kuzingatia Katiba na kanuni za chama na hao wanaosema mimi ni dikteta, hakuna jambo kama hilo.

Vyama vinne vyasajiliwa
Katika hatua nyingine, ikiwa imebaki miezi minane kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, vyama vinne vya siasa vimewasilisha barua ya maombi ya usajili katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, huku vingine viwili vikipatiwa usajili wa muda.

Vyama vilivyopata usajili wa muda ni; Chama cha Wananchi na Demokrasia (Chawade) kilichoasisiwa na Shabiri Mpaka na Pilly Athuman na Chama cha Maridhiano na Uwiano (CMU) chini ya waasisi Jamali Abdallah na Shaibu Hemed Likwimbi.

Chama cha Kijamii na Uzalendo Tanzania (CKUT), chini ya waasisi wake Ramadhan Semtawa na Noel Antapa kiliwasilisha maombi yake Januari 6. Vingine vilivyowasilisha barua ya maombi tangu mwaka jana ni; Chama cha Demokrasia na Umoja (Dau) ambacho waasisi ni Idd Mwishwa na Lazaro Mwalusamba, Restoration of the National (RNP) chini ya waasisi Atis Jacob Atto na Jenesta Josia na True Conscious for Liberation (TRUCOLI) ambacho kimeasisiwa Leonard Nyongani na Boniface Magesa.

CHANZO:MWANANCHI
Toa maoni yako kwa habari hii kwa kuweka email yako hapa,na endelea kutufatilia zaidi Ukurasa wa habari

0 comments:

 
Supported by AMAGA Media services : | |
Copyright © 2015. UKURASA WA HABARI - All Rights Reserved
Templete Designed by Abdallah Magana
Proudly powered by Blogger